MCHAKATO WA KUIGEUZA BODI YA UTALII KUWA MAMLAKA YA UTALII UHARAKISHWE– BALOZI MULAMULA
Balozi
wa Tanzania nchini Marekani Mh. Liberata Mulamula ametoa rai kwa vyombo
vinavyohusika kuharakisha mchakato wa kuigeuza Bodi ya Utalii (TTB)
Tanzania kuwa Mamlaka ya Utalii Tanzania ili kukiwezesha chombo hili
kuwa na uhuru zaidi na uwezo mkubwa katika kutangaza vivutio vya utalii na kusimamia sekta ya utalii nchini.
Hayo
yalisemwa na Balozi Mulamula hivi karibuni alipomtembelea Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Dk. Aloyce K. Nzuki ofisini kwake
ili pamoja na mambo mengine kuzungumza namna gani Ubalozi wa Tanzania
nchini Marekani utasaidia juhudi za TTB katika kutangaza vivutio vya
utalii vya Tanzania katika soko la Marekani.“Ni muhimu ifike mahali TTB
iwe na nguvu kisheria na uwezo zaidi katika kutekeleza majukumu yake
bila kuingiliwa au kuwepo kwa migongano, hivyo ni vema mchakato huo wa
mageuzi ukaharakishwa” alisema Balozi Mulamula.
Akifafanua
zaidi kuhusu suala hilo Dr. Aloyce Nzuki alisema tayari Bodi ya Utalii
ilikwishaandaa andiko kuhusu kuigeuza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa
Mamlaka ya Utalii Tanzania (TTA) na andiko hilo kwa sasa liko Wizarani.
Aidha balozi Mulamula ameipongeza TTB kwa kubuni onesho la utalii liitwalo Swahili International Tourism Expo
(S!TE) litakalo kuwa likifanyika kila mwaka mwezi Oktoba ambalo
litatumika pia kuonesha utamaduni wa mwambao na kukuza lugha ya
Kiswahili. Ameahidi kuweka kiunganisho (link) cha tovuti ya onesho hilo
la S!TE katika tovuti ya Ubalozi. Sambamba na hilo amesema pia kuwa
kuanzia mwaka huu ofisi yake ambayo imekuwa ikiandaa na kuratibu safari
ya wafanyabiashara mashuhuri wa Marekani kutembelea Tanzania (VIP Safari)
sasa itakuwa ikiandaa safari hiyo na kuwaleta wafanyabiashara hao mwezi
Oktoba wakati wa onesho hilo la S!TE badala ya utaratibu wa zamani wa
kuwaleta wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es salaam
maarufu kama Sabasaba.
Ameahidi
kuwa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani utafanya kila liwezekanalo
kusaidia juhudi za TTB katika kuitangaza Tanzania kama eneo zuri la
utalii duniani na akaiomba TTB kuendelea kuwapa taarifa mbalimbali za
vivutio vya utalii kadri iwezekanavyo ili kuwasaidia kutekeleza azma
hiyo.
Leave a Comment