Uhuru wa vyombo vya habari mashakani: Afrika
Ripoti ya Shirika la maripota wasio na mpaka mwaka 2014 linasema
migogoro barani Afrika imezidisha hatari kwa uhuru wa kujieleza,
likisema hali hiyo imedhihirika bayana nchini Mali na katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati.
Ripoti ya mwaka 2014 kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, hususan barani
Afrika, inajikita juu ya namna migogoro mipya barani humo inavyoambatana
na changamoto za kipekee juu ya uhuru wa habari. Kwa mfano, baada ya
wanajeshi kuiangusha serikali ya Mali mwaka 2012, hatua ya kwanza
waliyoichukua ilikuwa kukiteka kituo cha taifa cha Televisheni na radio.
Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, makundi yenye mielekeo ya
kisiasa hutumia silaha za kivita kujinufaisha kiuchumi, na hujitahidi
kudhibiti vyombo vya habari kwa maslahi yao. Mfano unaotolewa ni wa
kundi la waasi wa M23, ambalo ripoti hiyo inasema liliyakagua magazeti
kabla ya kuruhusu yasambazwe katika maeneo lililokuwa likiyashikilia, na
liliwatisha mameneja wa vituo vya radio ambavyo vilitangaza habari
ambazo zililikosoa kundi hilo.
Mizozo mipya ya kisiasa
Katika Jamhuri ya Afrika Kati, ambako hakukuwa na mshindi wa
dhahiri kati ya muungano wa makundi ya waasi wa Seleka na wanajeshi
waliomtii rais aliyepinduliwa na Seleka, Francois Bozize, maafisa wakuu
wa polisi waliwahoji wenyewe na kuwatisha waandishi ambao walidiriki
kuzungumzia uwezekano wa kulifanyia marekebisho baraza la mawaziri.
Ripoti hii inaeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari uliendelea kudidimia
katika eneo zima la Afrika ya Kati, kuanzia nchi za mwambao wa Bahari
ya Atlantiki hadi kanda za maziwa makuu. Inasema hali ni mbaya zaidi
katika Guinea ya Ikweta, nchi pekee inayozungumza kihispania katika eneo
hilo. Ripoti inasema hakuna mwandishi hata mmoja aliyeripotiwa
kunyanyaswa, kwa sababu wote wamezibwa mdomo, na kwa hivyo ama hujiwekea
mipaka wenyewe, au huikimbia nchi.
Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mgogoro wa umwagaji damu umeyafanya
magazeti yaegemee upande mmoja na kuchochea vurugu zaidi kuliko kuupasha
umma habari za kuaminika. Nchini Chad, ambako uongozi ni wa kiimla,
waandishi 23 wa habari walikamatwa mwaka 2013, na ingawa waliachiwa
baadaye, lakini hawakuweza tena kutangaza habari kwa njia huru. na huko
Angola, mwandishi wa habari Rafael Marques de Morais amekamatwa na
kuhojiwa mara kadhaa, baada ya kuchapisha kitabu kinachochambua maovu
yanayofanywa katika sekta ya almasi nchini humo.
Kundi la Boko Haram huuwa waandishi na kuharibu magazeti
Burundi imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya chini juu kutunga sheria zinazokandamiza zaidi uhuru wa vyombo vya habari.
Mwiko kuitaja Boko Haram
Kwingineko barani Afrika, kundi la Boko Haram nchini Nigeria ambalo
linashukiwa kuwa na mafungamano na mtandao wa al-Qaida, linatajwa katika
ripoti hiyo kwamba liliwauwa waandishi wawili walioandika taarifa
ambazo lilizichukuliwa kuwa si sahihi, na limeyaharibu magazeti kwa
kuyapiga mabomu
Katika eneo la pembe ya Afrika, Eritrea imeelezwa kuwa gereza kubwa kwa
waandishi wa habari kwa kuwa na waandishi 28 wanaosota jela, nako nchini
Somalia, waandishi wanaojaribu kutoa taarifa zisizoegemea upande wowote
wamejikuta wakiwindwa na pande zote, yaani serikali na waasi wa
al-Shabaab. Mwaka 2013, waandishi saba waliuawa nchini humo.
Hata hivyo ripoti hiyo inafurahia kuibuka kwa teknolojia inayowawezesha
watu kupata habari kupitia njia nyingi zaidi, tofauti na siku za nyuma
ambako radio na magazeti ilikuwa njia pekee y kupata habari. Daniel
Gakuba anakupasha zaidi katika taarifa ifuatayo.
Leave a Comment