JINSI YA KUEPUKA UGONJWA WA KISUKARI

Kisukari Ni Nini?
Kisukari ni ugonjwa unaotokana namtu kuwa na sukari nyingi kupita kiasi kwenye damu. Ugonjwa huo huvuruga utaratibu wa kuingiza sukari ndani ya chembe kutoka kwenye damu kwa kuwa chembe huhitaji sukari ili kupata nishati.
Matokeo ni kuharibiwa kwa viungo muhimu na hitilafu ya mzunguko wa damu, na nyakati nyingine unaweza kufanya mtu akatwe vidole vya miguu au mguu, pia husababisha upofu, na maradhi ya figo.

Wagonjwa wengi wa kisukari hufa kutokana na mshtuko wa moyo au kiharusi.

UGONJWA wa kisukari unaongezeka haraka sana hivi kwamba umekuwa janga la ulimwenguni pote. Kuna aina mbili kuu za kisukari. Aina ya kwanza huanza hasa utotoni, na kufikia sasa madaktari hawajui jinsi ya kuizuia.
Makala hii inazungumzia aina ya pili, ambayo imeathiri asilimia 90 ya watu walio na kisukari. Ingawa zamani aina ya pili ya kisukari ilihusianishwa tu na watu wazima, hivi karibuni imewaathiri pia watoto. Lakini wataalamu wanasema kwamba mtu anaweza kujikinga ili asipatwe na kisukari. Huenda ukafaidika kujua habari Fulani kuhusu ugonjwa huu hatari.

Mafuta mengi kupita kiasi mwilini huchangia sana kisukari. Wataalamu wanaamini kwamba mafuta yaliyokusanyika tumboni na kiunoni ni ishara ya uwezekano wa kupatwa na kisukari. Kihususani, mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu. Unawezaje kuepuka kupatwa na kisukari?
Hatua Tatu Zinazoweza Kukusaidia Usipatwe na Kisukari
1.    Pimwa kiwango cha sukari kwenye damu ikiwa una uwezekano mkubwa wa kupata kisukari.
Mara nyingi aina ya pili ya kisukari huanza baada ya hatua inayoitwa prediabetes,yaani, ongezeko la kiwango cha sukari kwenye damu.
Hatua hiyo ni hatari kama tu kisukari, lakini kuna tofauti: Ingawa ugonjwa wa kisukari unaweza kudhibitiwa,
hauwezi kutibiwa. Kwa upande mwingine, watu walio na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu wamefaulu
kukipunguza. Huenda mtu asitambue dalili za ongezeko la sukari kwenye damu. Kulingana na ripoti mbalimbali,
karibu watu milioni 316 duniani pote wana kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu; ingawa wengi wao hawajui wana kiwango hicho. Kwa mfano, nchini Marekani pekee asilimia 90 ya watu wenye sukari nyingi kwenye damu hawatambui kama wana tatizo hilo.
Ingawa hivyo, ongezeko la sukari kwenye damu ni hatari. Mbali na kuwa kisababishi cha kisukari, hali hiyo imehusianishwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa akili uitwao dementia. Kama wewe ni mnene kupita kiasi,
hufanyi mazoezi kwa ukawaida, au una watu wa ukoo walio na kisukari, huenda tayari una kiwango cha juu cha sukari kwenye damu. Unaweza kujua kiwango chako cha sukari ukipimwa damu.
2. Kula vyakula vyenye lishe.
Unaweza kufaidika ukifanyamamboyafuatayo: Punguza kiasi cha chakula unachokula.nBadala ya kunywa vinywaji vyenye sukari nyingi au vinywaji vyenye kaboni kama vile soda, kunywa maji, chai, au kahawa. Kula vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa badala ya vyakula vilivyochujwa sana viwandani. Kula nyama isiyo na mafuta mengi, samaki, njugu, karanga, na maharagwe.

3. Fanya mazoezi.
Kufanya mazoezi kunaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na kukusaidia uwe na uzito unaofaa. Mtaalamu fulani anapendekeza kupunguza muda unaotumia kutazama televisheni ili uwe na muda wa kufanya mazoezi. Huwezi kubadili chembe zako za urithi, lakini unaweza kubadili maisha yako. Utafaidika sana ikiwa utajitahidi kutunza afya yako

‘NILICHUKUA HATUA!’
Mahojiano
Ulijuaje kwamba ulikabili hatari ya kupatwa na kisukari?
Nilipofanyiwa uchunguzi wa kitiba kabla ya kuanza kazi mpya, daktari aliniambia ningepatwa na kisukari ikiwa nisingechukua hatua. Nilikuwa na mambo manne yanayochangia kisukari:
Nilitoka kwenye jamii ya watu wanaopatwa sana na kisukari, watu wangu wa ukoowalikuwa na kisukari, nilikuwa mnene kupita kiasi, na sikufanya mazoezi. Kwa kuwa singebadili mambo mawili ya kwanza, niliamua kurekebisha mambo mawili ya mwisho.
Ulifanya nini?
Nilienda kumwona mtaalamu wa kisukari ambaye alinifafanulia uhusiano kati ya vyakula, mazoezi, uzito,
na kisukari. Niliamua kubadili maisha yangu. Nikaanza kula mboga kabla ya kula chakula kingine. Hilo lilinipunguzia njaa hivyo sikula sana. Pia, nilianza kufanya mazoezi, jambo ambalo nilikuwa nimepuuza kwa miaka mingi.
Je, ulifaulu?
Kwa kipindi cha miezi 18, nilipunguza asilimia kumi ya uzani wangu, na ninahisi vizuri sana. Nimeazimia kwamba sitaishi tena kama zamani. Hupaswi kucheza na kisukari!

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.