MGANGA WA KIENYEJI ANASWA NA FUVU LA BINADAMU LIKIWA NA NYWELE
Wakati kamatakamata ya waganga wa
kienyeji ikiendelea kupamba moto katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, mmoja
amenaswa akiwa na viungo vya binadamu, kikiwemo kichwa ambacho bado
kilikuwa na nywele zake.
Mganga huyo, Nyamizi Makunga (70),
mkazi wa Kijiji cha Igurubi wilayani Igunga, Tabora, alitiwa mbaroni
juzi. Mbali na viungo hivyo, pia alikutwa na vifaa vingine, zikiwemo
nyara za serikali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Igurubi,
George Henry, alisema Makunga alikamatwa nyumbani kwake kutokana na
msako mkali unaendelea kwa lengo la kuwabaini waganga wanaofanya ramli
chonganishi.
Msako huo umetokana na kukithiri kwa
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ambapo serikali katika kubaini
chanzo, imekuwa ikisaka waganga wanaotuhumiwa kufanya ramli hizo.
Henry alisema polisi walifanikiwa
kumnasa Makunga kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema, ambapo
walipofanya msako walikuta fuvu la kichwa la binadamu likiwa na nywele
zake.
Mbali na fuvu hilo, polisi pia walikuta
kipande cha mfupa wa binadamu, mkia wa nyumbu, gamba la kobe na ngozi
za wanyama mbalimbali.
Wananchi wa Kijiji cha Igurubi,
wamepongeza msako unaofanywa na polisi kuwatia mbaroni waganga ambao
ndio chanzo cha kushamiri kwa mauaji ya albino.
Pia walisema kwa muda mrefu Makunga
amekuwa kikwazo cha maendeleo kwenye eneo hilo kutokana na kufanya mambo
kinyume na kwamba wananchi wamekuwa wakimwogopa.
Alipohojiwa, Makunga alikiri viungo hivyo ni vya binadamu na kuwa aliachiwa na baba yake ili kuendesha shughuli za uganga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, alithibitisha kukamatwa kwa mganga huyo akiwa na viungo vya binadamu.
Leave a Comment