STRESS ZA MAPENZI HAZIPUNGUZWI KWA KUCHEPUKA!

Image result for michepuko

LABDA haijawahi kukukuta, lakini maisha tunayoishi katika wakati wa sasa yanasababisha watu wengi wanapatwa na msongo wa mawazo, maarufu kama stress. Hali ni mbaya kwa wafanyakazi wenye mabosi wakorofi na hata wafanyabiashara wanaoyumba kiuchumi.

Lakini inakuwa mbaya zaidi mambo yanapoharibika ndani ya familia, kwa maana ya wanandoa au walio katika uhusiano wa kimapenzi. Ingawa sina takwimu kamili, lakini uzoefu unaonyesha tafrani katika ndoa zinasababisha watu wengi sana kuchanganyikiwa na hata kusababisha kukosa amani ndani ya mioyo yao.

Na siyo kukosa amani na kuchanganyikiwa tu, wengi pia wamepoteza maisha baada ya kushindwa kuhimili mikanganyiko iliyotokea. Mtu anaona mwenzake anakwenda ndivyo sivyo katika uhusiano wake anaamua kujimaliza mwenyewe, achilia mbali wanaoamua kujimaliza wote ili kila mmoja akose.

Ukiachana na hawa wanaokosa uvumilivu, kuna wale ambao badala ya kufanya vitu kama hivyo, wao huamua ‘kuchepuka’ ili kupunguza stress zinazotokana na mikwaruzo katika familia. Yaani ili mama aondoe ‘hasira’ za baba kumzingua jana yake, anachofanya ni kumkumbuka mtu wake wa zamani, mume wa mpangaji mwenzake aliyemkonyeza jana, jirani yao nyumba ya pili au hata kiserengeti boy chake na kwenda kuburudika nacho.

Anafanya hivi kwa akili zake akiamini kuwa anajisahaulisha machungu au kama wengi wanavyochukulia kuwa wanawakomoa wenza wao. Wachepukaji wenzao wakiwauliza vipi kuhusu waume zao, ni rahisi kuwabeza na kuwadharau!

Hali kadhalika akina baba nao baada ya kushindwa kuelewana na wake zao, kinachofuata ni kuangalia katika orodha ya walio katika simu na kumkumbuka Mwajuma Ndala Moja, jirani anayejigonga kila siku, mfanyakazi mwenzake ofisini au hata dada wa dukani anayemchekeaga akienda kupata mahitaji.

Image result for michepuko
Akienda huko, hata anaochepuka nao wanapojaribu kujifanya kumuogopa mkewe au rafiki yake, ni rahisi kukutana na majibu kama haya; “achana naye mjinga huyo, wewe tulia kula maisha” au “Anajifanya anajua wakati anaungua na jua, achana naye.”

Lakini unapojaribu kuangalia suala hili, unajikuta unagundua kwamba hakuna yeyote kati yao ambaye kwa kweli anaondoa stress zaidi ya kuongeza matatizo. Utakwenda nje, sawa, lakini kumbuka huendi kule baada ya kumbusu na kumdanganya mwenzio, bali unakwenda ukiwa umenuna na hutaki hata kuaga unakoenda.

Matokeo ya uchepukaji wa namna hii ni kukosa uangalifu na umakini katika ufanyaji wa tendo, kitu ambacho kinaweza kuleta athari, siyo tu kwa mhusika, bali hata kwa mtu wake aliyemuacha nyumbani.
Ukiachana na athari za kiafya kwa mfano, lakini hata lugha ya dharau kwa mwenza wako unayoitoa, nayo inaweza kuleta madhara kwa upande wa pili kwa sababu tayari watu wa nje wanatambua udhaifu uliopo ndani mwenu. Yule jirani uliyechepuka naye atatangaza kwa marafiki zake juu ya ugomvi wenu na jinsi ulivyomdharau mume au mke wako.

Hiyo itasaidia kuzidi kumdharaulisha mume au mke wako mtaani kwenu kwa sababu watu watamuona mwenzako kama mtu rahisi na asiye na maana. Kitu cha msingi unachopaswa kufanya kila inapotokea kutoelewana ndani ya nyumba au uhusiano wenu, unatakiwa kuwa mtulivu kiakili kuliko wakati mwingine wowote.

Kumbuka, huu ni wakati unaoweza kufanya kosa linaloonekana dogo, lakini likakupa madhara makubwa. Unapohitaji kupata muda wa kujiuliza, basi usiweke mambo ya ngono akilini mwako. Tafuta mtu unayemuamini na kumwelewa, mshirikishe tatizo lako. Faida ya kumshirikisha mwingine katika tatizo lako ni zuri kwa kuwa mawazo mawili matatu tofauti kutoka vichwa tofauti yatakupa mwanga wa kujua nini cha kufanya ili kukabiliana na kilicho mbele yako.

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.