MAPENZI SIYO HISIA, NI UHALISIA!

KUNA watu wanaweza kupatwa na mshangao kwa kichwa cha habari hapo juu. Watajikuta wakishangaa kwa sababu siku zote wamekuwa wakielewa kuwa mapenzi ni hisia, kwa sababu yanamwendesha mtu vile anahisi. Leo nataka kuwahakikishia kuwa kamwe, jambo hili siyo hisia, bali ni uhalisia!


Inaweza kuwa vigumu kuelewa mara moja maana yangu, lakini kuna mifano rahisi na mifupi ninaweza kukupa ili uelewe maana yangu. Kunywa maji wakati ukiwa na kiu siyo hisia, bali ni uhalisia, kutakiwa kuogelea ukiwa ndani ya maji ni uhalisia, siyo hisia!

Ni kama vile ambavyo ukiwa umechoka na kuhitaji kujipumzisha kwa kulala kidogo, zile siyo hisia, ni uhalisia, ingawa unaweza kusema unajisikia vizuri kwa kujilaza. Hisia ni vitu vinavyotokana na tafsiri pamoja na uzoefu, wakati uhalisia hauhitaji tafsiri, bali ni vitu ambavyo vipo, vipo sawa na vinasomeka.

Kinachotokea ni kwamba sisi, kwa sababu ya kujiridhisha, tunatafsiri mapenzi yetu na kuyafanya kuwa hisia. Mwanaume kumhitaji mwanamke siyo suala la hisia, ni uhalisia, kama ilivyo kwa mwanamke anapomhitaji mwanaume. Kama kuna mtu anaweza kubisha kuhusu hili, basi sitahitaji kubishana naye kwa sababu ninajua sitaweza, isipokuwa nitaomba msaada wako wewe msomaji, ni kweli unamhitaji mwenza wako kwa sababu ya hisia zako au uhalisia wako?

Hisia zinabadilika kulingana na wakati, hakuna inayodumu kwa muda mrefu. Unaweza ukampenda mtu kwa dhati leo, lakini kesho au mwezi ujao ukamwondoa mawazoni. Labda kama hisia zako zitakuwa ni za kujiuliza ni vipi kwa uzuri wote ule umebadilika haraka kiasi hicho!

Mwisho wa hisia, hugeuka kuwa kinyume chake. Kwa mfano, hisia zenye mvuto mkubwa wa mapenzi, upendo na furaha, hugeuka kuwa chuki, hasira na kutokuelewana. Hapo ni pale hisia zinapokuwa zimepoteza mwelekeo unaotokana na maisha yanayoendelea wakati huo. Wakati hili linafanyika, kwa maana ya hisia za mwenza mmoja kubadilika, haziondoi uhalisia wa mahitaji yake ya jinsia nyingine katika maisha yake ya kimapenzi.


Kitu cha muhimu ninachotaka kubadilishana mawazo na wewe msomaji wangu ni kwamba, katika mapenzi, tunao uhalisia wa mahitaji na tunazo hisia za mahitaji. Mwanaume anaweza kuwa na uhalisia wa kuhitaji kukutana na mwanamke, lakini hisia zinamlazimisha kumtafuta mwenye kuendana na vigezo vyake.
Kwa mfano, Ben ni kijana anayependa wasichana wenye makalio makubwa, akiwapata, yupo tayari kupoteza kiasi chochote cha fedha alichonacho ilimradi awe nao wa aina hiyo.

Lakini kumbuka, ingawa anawahitaji wa namna hiyo, hiyo haina maana kuwa hawezi kushiriki na wasichana wenye muonekano tofauti kwa muda wote ambao wa vigezo vyake watakosekana. Hisia zitakaposhindwa kukamilika, itabidi Ben awe katika uhalisia, wa kuhitaji mtu wa kuwa naye kwa muda huo!

Lengo la mada hii ni kuwakumbusha kuwa katika maisha yetu ya kimapenzi, tunavyo vitu vya lazima ambavyo tunatakiwa kuwa navyo na vipo vitu ambavyo si vya lazima, lakini vinasaidia kulifanya penzi letu kuwa katika sura tunayohitaji.

Kila mmoja angehitaji kuwa na mwenza wake na katika hilo, yapo mahitaji ya msingi ambayo mume au mke ni lazima ayapate, bila kujali mbwembwe. Vitu vya lazima vya kimapenzi vinazungumza kuhusu kutoka kwenda matembezini siku za mwisho wa wiki, lakini havitaji eneo gani. Hali ya maisha ya wapendanao inaamua kuhusu wapi kwa kwenda!

Kutoka kwenda matembezini ni jambo la lazima kwa wapendanao ili kubadili upepo, lakini kwamba ni lazima kwenda katika hoteli kubwa, hizo ni hisia zisizo na uhalisia!

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.