Vyombo vya Habari vyakumbushwa Maadili

Tasnia ya habari ni taa ya umma inayomulika na kuangaza kwenye giza na kuonyesha wazi yaliyojiri humo pamoja na kufichua maovu kwa faida na maslahi ya umma.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari kuhusu namna ya kuandika na kufuatilia habari za uchanguzi mkuu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora Thomas Mgaiya amesema baadhi ya wanahabari wanatumia kisingizio cha maslahi duni kama kigezo cha kuomba rushwa ili kuzima masuala nyeti katika jamii.
Amesema taa hii ikizimwa taifa litakuwa kwenye giza la rushwa na maovu kwa sababu hakuna wa kuyamulika na kuyakemea tena.
Ameongeza kuwa kwa bahati mbaya taa hii inapendwa na watu wachache wapenda haki ila kwa waovu wanaiona kama inawazibia njia.
Bw. Mgaiya amesema Wanahabari wamefanikiwa kufichua mambo yanayolitafuna taifa hili na hivyo kudhoofisha uchumi wake kukua, ukimlenga mwananchi wa kawaida, hata hivyo kazi hiyo nzuri bado inadhoofishwa kwa vikwazo mbalimbali.
Akitoa mada kwa kutumia mifano hai Bw. Mgaiya ameeleza kuwa kuna usemi kwamba, “Huwezi kula vidole vinavyokulisha”. Kumbe kama watenda maovu wataendelea kuwalisha na kuwanywesha wanahabari, ukweli utakuwa umeuawa.
Ukweli siku zote unauma, waandishi wanaokula rushwa hawataweza kuwauma wala rushwa wenzao kwa sababu na wao wamepata mgao.
Hivi ndivyo tasnia ya habari inavyoenda kuzimika kama kibatari katikati ya upepo mkali wa rushwa, vitisho, mauaji ya waandishi, kutekwa na kujeruhiwa vibaya.
Sote tunakumbuka yaliyomkuta ndugu yetu hayati Daudi Mwangosi, aliyeuawa kikatili katika mikono ya polisi, Absalom Kibanda alivyokamatwa na kuteswa vibaya hadi kutobolewa jicho lake. Tunamkumbuka pia Saed Kubenea alivyomwagiwa tindikali machoni na Ndimara Tegambwage alivyokatwa mapanga.
Yote haya yanadhihirisha kuwa kazi ya uandishi wa habari haimfurahishi kila mtu. Wanaosema ukweli wanawindwa na wanaosema uongo wanalindwa.
Mambo haya yanafanywa na wasiopenda mwanga wa tasnia hii. Wanaopenda giza, maovu yao yasimulikwe kamwe, wako tayari kuyafunika kwa gharama yoyote hata ikibidi kumwaga damu za watu.
Leave a Comment