KAMA UNAOGOPA KUUMIZWA KATIKA MAPENZI, SOMA HAPA!

Ni jambo lisilofichika kuwa wapo watu wengi wanaogopa kuumizwa katika mapenzi. Kuumizwa huku kunaweza kuwa kwa namna kadhaa kama vile kumpenda mtu halafu mtu husika asionyeshe kukujali, au kuwa katika mahusiano na mtu halafu mtu huyo baada ya muda fulani akakuacha na kuenda zake na mpenzi mwingine.
Kwa mtazamo huu watu wanaogopa kuumizwa katika mapenzi wapo wa aina mbili; wale ambao wanaogopa hata kuwa na mpenzi kwa sababu ya kuogopa kuumizwa, na wale ambao wapo katika mapenzi lakini hawaamini kama wapo salama, maisha yao ni ya wasiwasi kuwa muda wowote mpenzi anaweza kumuacha ‘solemba’.
Makala hii inachambua namna ya ‘kudeal’ na hofu ya kuumizwa katika mapenzi.

Sababu za kuogopa:
Mambo kadhaa yanaweza changia mtu kuogopa kuumizwa katika mapenzi. Zifuatazo ni baadhi:
  • Mtu alishawahi kuachwa ‘solemba’ na mpenzi hapo kabla
  • Mtu ameshuhudia rafiki, ndugu au jirani akiachwa ‘solemba’
  • Wivu uliopitiliza kwa mpenzi husika bila kuwa na sababu za msingi za wivu.
  • Kuishi kwa kufuata matarajio ya watu wengine:Yaani mtu yupo katika mapenzi lakini ni kama vile anaripoti mambo yake ya mapenzi kwa watu wengine. Hivyo anaogopa ‘jina’ lake litachafuliwa endapo itaonekana mpenzi kamuacha.  Kwani kwa wengine kuachwa katika mapenzi kunamaanisha udhaifu wa kutokufanikiwa katika maisha.
  • Kumtegemea sana mpenzi , hususani kumtegemea kifedha:  Hii hutokea pale mtu anapoamini na kuishi kuendana na imani yake kuwa mpenzi wake ndiye ‘kila kitu’ katika maisha. Wapo wanaotegemea wapenzi wao kwa kila kitu kuhusiana na elimu yao (msaada wa materials, kuandika reports, n.k), wapo wanategemea wapenzi wao kwa kila kitu kuhusiana na matumizi yao –chakula , mavazi, n.k

Mambo ya msingi ya kuzingatia kushinda hofu ya kuumizwa
1.Uoga hausuluhishi tatizo:  Kuogopa kuwa utaachwa au hautapendwa vile unavyotarajia kupendwa hakuleti suluhu ya hofu yako. Tumia muda kutambua chanzo cha hofu yako ni nini haswa. Jipe muda kumfahamu mpenzi unayetaka kujenga nae mahusiano, au yule ambaye tayari upo nae. Jishushe vya kutosha ukiamini kuwa wewe ni sehemu ya suluhisho ya tatizo. Hivyo tambua namna tabia yako, matarajio yako, na uelewa wako kuhusu mahusiano kunavyoweza kuchangia kuboresha mahusiano ili usiumizwe.
2.Binadamu kwa kawaida ni mbinafsi:  Kwa asili binadamu huangalia maslahi yake , na kuwa angependa kunufaika zaidi na zaidi. Hivyo angalia namna unavyoendesha mahusiano kama kweli unampatia sababu mpenzi wako kuona ananufaika zaidi na zaidi. Je, kuna mambo anayoyalalamikia kwako na ungeweza kuyarekebisha? Je, unaboresha mawasiliano kati yenu ili kujua hisia kati yenu?Je unazungumzia mambo unayohofia na yale usiyoyapenda?
3.Chunguza matarajio yako kuhusiana na mahusiano : Tusipokuwa makini kuhusu yale tunayoyatarajia katika mahusiano  tunaweza kujikuta tunawapoteza wapenzi wetu, kwani pengine matarajio yetu ni zaidi ya uwezo wa wapenzi wetu au pengine yanapingana kwa kiwango kikubwa na matarajio ya wapenzi wetu.  Mfano uharaka wa kutaka mpenzi wako ajenge, alipe mahali,  akununulie mali kadhaa n.k vinaweza kumpoteza. Chukua muda kujifunza hali halisi ya mpenzi wako, na kanuni za kimaisha anazoziamini.
4.Ishi wewe kama wewe:  Usiige maisha ya watu na wala usitake kujionyesha mbele za watu kuwa wewe ni bora kutokana na aina ya mpenzi uliye naye, au kwa vile ‘unavyo enjoy’ maisha. Mapenzi yako ni kwa ajili yako. Unapoanza kuingiza mitazamo ya watu wengine au kutaka ‘kuwauzia sura’ watu wengine mapenzi yako, unatengeneza deni ambalo matokeo yake ni kujikuta unaishi kwa hofu ya kuachwa na uliye naye, kwani kuachwa kwako kutakuumiza zaidi kwa kuwa kutakuaibisha mbele ya watu wengine.

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.