STORI ITAKAYOKUFANYA UJIONE UMECHELEWA
Umakini unahitajika sana hasa pale mwanaume unapotafuta mwanamke wa
kuanzisha nae maisha, simulizi hii nimeiona mahala nikaona bora nijaribu ku
share nanyi.
Desemba 22, 2007. Jumamosi.
Victor, akiwa na miaka 36, alikuwa akifunga ndoa. Ilikuwa ni siku ya
sherehe hoi hoi nderemo na vifijo kwani wengi wetu tulikuwa tumeshahisi kuwa
kaka Victor hatooa tena. Kila siku alikuwa akituambia kuwa anajipanga na
maisha, na anawaandalia watoto wake maisha mazuri.
Tulibaki tukijiuliza hao watoto wako wapi maana hatuoni hata dalili za yeye
kuwa na ukaribu na mabinti hata wa jirani.
Kaka Victor kwa jina lingine Mchungaji ni katika wale wakaka ambao wakati
tunakua walikuwa ndio wakaka wa kutolewa mifano majumbani mwenu (role models).
Yaani ukifanya jambo baya au kosa unaambiwa, “Muangalieni kaka yenu, kwa nini
msimuige hata robo tu ya tabia zake?”
Kuna kipindi rafiki yake aliwahi kuniambia, “Yani siku nikimkuta mchungaji
Victor na mwanamke chumbani na wote wako uchi na mchungaji akaniambia,
sijamfanya chochote, nitamuamini”
Hivyo ndivyo jinsi kaka Victor alikuwa amejijengea sifa katika jamii. Zaidi
ya yote, kaka Victor alikuwa mfano wa kuigwa hata kimasomo kwani baada ya
kumaliza shahada yake ya kwanza katika masomo ya uchumi na kufaulu vyema,
alibahatika kupata ufadhili wa kwenda kusoma masomo ya shahada ya uzamili
katika chuo kikuu cha Havard huko Massachussets, nchini Marekani.
Alikuwa na akili ya peke yake na mtu wa kujituma. Kwani alipomaliza chuo
yeye kabla hata chuo kikuu cha Dar es salaam hawajamuita kuwa mkufunzi msaidizi
alikuwa ameshajiajiri kwenye kampuni yake ndogo ya BIMA.
Ngoja nikurudishe nyuma kidogo; wakati yuko mwaka wa pili chuoni yeye
pamoja na mwenzake waliandika proposal ambayo ilishinda na walipewa kila mtu
fedha taslimu shilingi milioni tano. Katika vitu alivyovifanya ilikuwa kununua
kiwanja huko Kigamboni jijini Dar es salaam, eneo kubwa huko ambako kwa sasa
kuna kijiji kiitwacho Avic town.
Fedha nyingine alianzisha ‘agency’ yake ya mambo ya BIMA. Ni wakati
anajiandaa kwenda kusoma nje alipofuatwa na wawekezaji waliojenga hiyo Avic
town ili wanunue eneo lake kwani lilikuwa limepakana sana na eneo lao.
Kwa fedha zile aliwekeza zaidi kwenye ‘agency’ yake na kuongeza mtaji hadi
kufanikiwa kuwa ‘brokerage’. Pamoja na yote hayo alikuwa na vibiashara vya hapa
na pale ambavyo vilifanya maisha yake mjini hapa kuwa mazuri na alizidi
kutufanya wadogo zake sisi tuonekane bado sana.
Kaka Victor alikuwa mcheshi na mchangamfu na kama kawaida wadada wengi
walijisogeza kwake lakini nahisi katika mambo yaliyokuwa mwishoni mwa mawazo
yake ni hilo la wanawake.
Kila alipokuwa akiulizwa suala la mahusiano alijibu, tena kwa kizungu, “I
worry about things that I have to struggle for, not those that are provided by
nature” akimaanisha yeye anahofia juu ya mambo ambayo inabidi kuyapigania
kuyapata na sio yale ambayo yapo tu.
Kwamba siku mtu akitaka kuoa ataoa tu lakini huwezi kutaka kuwa na mali na
ukawa nazo, lazima uweke bidii kuzipata. Akiulizwa na watu wazima zaidi kuhusu
ndoa alikuwa akijibu, “najipanga na kuwaandalia maisha wanangu."
Siku zote hakukosa jibu la kwa nini hakutaka kuoa na kwa hilo alifanikiwa
kwani alifanikiwa kuwa na biashara ambazo zilikuwa zinaenda vizuri, nyumba ya
kuishi na nyingine za kupangisha tena si kwa hela zetu za madafu, uwezo wa
kubadili magari japo si kwa kila siku n.k.
Siku kaka Victor anatuambia anataka kuoa hakuna aliyeamini, hata alipomleta
binti ambaye kwa hali ya kawaida wengi tungemkataa basi ilibidi tutafute
justifications (vihalalishi) za kuonesha kuwa anaweza kuwa wa tofauti.
Na siku ya Jumamosi, Desemba 22, 2007 kaka Victor alifunga pingu za maisha
huku akiwa kwa hakika amejiandaa na kujipanga vyema kwa ajili ya wanae ambao
sasa tuliona wanaweza kupatikana.
Kuanzia Januari 2009
Mafanikio yalizidi kumiminika kwa kaka Victor ambapo wakati huu Mungu
alikuwa amewabariki na mtoto mmoja, James. Ni wakati huu pia alipopata ufadhili
kwenda nchini Ufaransa kwa ajili ya shahada yake ya uzamivu.
Aliondoka akiwa na amani kabisa akijua kuwa kila kitu amekiacha kikiwa
katika mikono salama. Hadi wakati kaka anasafiri hatukuwa na ukaribu sana na
shemeji yetu – mke wake – kwani hakupenda sana kututembelea na wala hakuwa
akipenda tukienda kwake.
Hata hivyo tulimheshimu kwani kaka alikuwa akimpenda sana na kumuamini.
Mwezi wa tano kaka alinipigia simu kuwa amepata safari kwenda jijini Rio de
Janeiro kwa ajili ya mkutano. Nilimtakia kila la kheri na hata alipofika
alinieleza jiji hilo lilivyo zuri na kunitumia baadhi ya picha kupitia barua pepe.
Juni, 1 2009
Nilipata habari kuwa ndege ya Air France iliyokuwa ikitokea Rio de Janeiro
kuelekea jijini Paris imepata ajali na abiria wote 216 waliokuwamo wamefariki.
Kwanza haikuniingia akilini hadi nilipokumbuka kuwa hiyo ndiyo siku ambayo kaka
alikuwa asafiri kurudi chuoni kwake huko Ufaransa.
Nilijikuta nikisali kumuomba Mungu kaka asiwepo kwenye ndege hiyo.
Nilijaribu kutumia njia mbalimbali kuhakiki kama alikuwepo bila mafanikio
yoyote. Ni hadi walipotangaza orodha ya abiria waliokuwa wamepanda ndege ile
ndipo tulipofahamu kuwa kaka Victor hatunaye tena duniani.
Mipango ya mazishi ilifanyika na kwa kuwa miili yao haikupatikana – kwani
ndege iliangukia baharini – tulifanya tu ibada na kila mtu kutawanyika.
Tulimuuliza shemeji kama aliacha wosia wowote na kama ilivyo ada hakuwa
ameandika chochote isipokuwa tu kwa kutumia fomu alizokuwa akijaza kazini na
kwingineko alikuwa akimuandika mkewe kama mrithi pekee wa mali zake endapo kifo
kitamkuta.
Hivyo sisi kwa kuamini walikuwa wanapendana hatukuona shida na tulimsaidia
kupata vibali vyote vya kuhakikisha mirathi na stahiki zote za mumewe anazipata
yeye. Tulimuonea sana huruma shemeji yetu kwani bado alikuwa binti mdogo.
Januari 6, 2016
Mpaka naandika hapa, shemeji yetu, aliyekuwa mke wa kaka yangu Victor, amehamia
nchini Uganda ambako ameolewa na mwanaume aliyekuwa akifanya kazi ubalozi wa
Tanzania nchini Uganda.
Miezi kama miwili tu baada ya kaka kufariki, shemeji alitokomea
kusikojulikana na kumuacha James mwanaye kwa mama yetu. Tulipojaribu kufuatilia
mali za mumewe alizoziacha tulikuta zote zimeshabadilishwa umiliki na hata
kampuni ndogo ile ya BIMA aliiuza kwa mchaga mmoja bila taarifa kwetu.
Hakurudi kumuangalia mtoto na hata alipokutana na ndugu yetu mwingine
alisema yeye ni mdogo mno kukaa peke yake na huyo mtoto anamnyima fursa hivyo
hatomrudia.
Ni jana tu ndiyo nilitoka kumlipia ada James ili aweze kuanza darasa la
kwanza mwaka huu. Hua najiuliza ni aina gani ya Mke kaka Victor alipata, yote
aliyokuwa akituambia kuwa anatafuta pesa kwa ajili ya mwanae ndio yameishia
hivi kwa sisi kumtunzia Mwanae. Juhudi na maarifa yake yote imekuwa bure
kabisa. Mwanae hatafaidi jasho lake hata kidogo.
KUMBUKA
MAISHA YANA MITIHANI MIKUBWA SANA JIFUNZE KUPITIA MITIHANI WANAYOPITIA
WENZAKO ILI SIKU UKIKABILIANA NA MTIHANI WOWOTE ULE UJUE NI JINSI GANI YA KUWA
MVUMILIVU NA KUWEZA KURIKABILI
Leave a Comment