Mahusiano ya kimapenzi yanavyoweza kuanzishwa bila kutarajiwa
Kwa kawaida, uhusiano huanza pale mtu anapovutiwa na mwingine iwe
kihisia au kimwili. Hiyo ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya mahusiano
ambayo hutegemea masuala makuu mawili.
Kwanza kabisa, ni ukaribu, propinquity. Tunaambiwa kwamba, watu wawili wanapojikuta bila hata wao wenyewe kutarajia katika mazingira ya ukaribu
iwe kwa kufanya pamoja kazi ofisi moja, kuabudu mahali pamoja, kusoma mahali panapofanana au kuishi mtaa
mmoja, huongeza uwezekano wa mmoja wao kuvutiwa na mwenzake na hivyo
kuanzisha mahusiano.
Tafiti zinathibitisha kwamba kadri unavyokutana na mtu iwe kwa kumwona
na kumsikia mara kwa mara, ndivyo unavyoongeza uwezekano wa kumpenda (liking)
na kwamba kwa kawaida, hatuvutiwi na vitu tusivyojua kwa karibu ikiwamo
watu. Kwa maana nyingine, kadri unavyokutana na mtu ndivyo unavyojikuta
ukiongeza evaluation ya kumpenda.
Kwa upande mwingine, ukaribu huu huongeza uwezekano wa kufanana mambo
fulani fulani kama imani na mitazamo na hivyo kuongeza ukaribu. Mfano,
vijana wanaokutana kanisani mara kwa mara kwenye ibada, mbali na
kuongeza uwezekano wa kuvutiana, lakini pia huongeza uwezekano wa watu
hao kuwa na imani, mitazamo na interests zinazofanana. Haya matatu huwa
ni kichocheo cha mvuto unaojenga mawasiliano ya kimapenzi.
Jambo la pili linaloanzisha mahusiano ni mvuto wa kimwili. Hapa tunazungumzia uzuri wa sura, urefu/ufupi, unene/wembamba, weupe/weusi na kadhalika. Sasa, uzuri ni relative.
Watu wanatofautiana namna wanavyotafsiri uzuri kutegemeana na
utamaduni, malezi, imani na sababu nyinginezo. Na wakati mwingine, uzuri
wa mtu hutegemea pia 'viwezeshi' vingine kama mavazi, mapambo,
anavyozungumza, anavyotazama na kadhalika.
Vyovyote vile iwavyo, wengi wetu huamini mtu mwenye mwonekano tunaouona sisi kuwa ni mzuri, basi automatically
huwa na haiba na tabia njema. Tuna mazoea ya kuhusianisha uzuri
unaoonekana na uzuri usioonekana. Ni aina fulani ya stereotype yenye
misingi yake kwenye malezi. Kwamba mzuri ana tabia nzuri jambo ambalo
hutufanya tutamani kuhusiana na watu tunaowachukulia kuwa wazuri.
Hata hivyo, tunaambiwa, pamoja na kwamba watu wengi hutamani kujenga
mahusiano na watu wenye mwonekano mzuri wa kimwili, mara nyingi huishia
kujenga mahusiano na watu wenye mvuto unaolingana na mvuto walionao wao
wenyewe. Unajikuta unahusiana na mtu anayefanana na wewe kwa kiasi
fulani. Ni hivyo mara nyingi. Ndio kusema, wanaotamani
kuhusiana na watu fulani wenye uzuri wa viwango fulani, hujikuta
wakihusiana na watu wa kawaida kama wao.
Bahati mbaya ni kwamba, mwonekano wa mwili huwa na nafasi kubwa katika
hatua za mwanzo za uhusiano na kuwa mahusiano ya kudumu huwa hayategemei
mvuto kama nitakavyoeleza katika aya chache zinazofuata. Lakini pamoja
na matatizo yake, uzuri wa sura na umbo una nafasi yake, kubwa tu, ya
kumfanya mtu ajiingize kwenye mahusiano.
Mambo yanayoendeleza mahusiano mapya
Wataalam wa mahusiano wanatuambia, baada ya mtu kuvutiwa na mtu fulani,
ni kawaida mtu huyo kufanya juhudi za kumvutia mtu huyo kwa kujaribu
kujenga taswira chanya ili naye avutiwe naye. Kanuni nne kubwa
zinazosaidia kuwafanya watu wawili waanze kuwa karibu kihisia, ili
waweze kuhusiana bila mikwaruzo, tranquility, ni haya yafuayo:
- Kwa kawaida, watu hujenga uhusiano na wale wanaowafanya wajisikie vizuri, yaani wanaowafanya wajisikie rewarded. Na kadri mtu anavyojisikia vizuri, ndivyo anavyovutiwa na wewe. Kinyume chake, ni kujisikia mzigo na hivyo kuongeza uwezekano wa mahusiano kwenda mbele. Kwa mfano, mwanamke hujisikia vizuri anapokuwa na mtu anayemfanya ajisikie kuwa mzuri na wa maana kama tulivyoona.
- Watu wana kawaida ya kukupa kile unachowapa, hivyo mtu anayeonesha kuvutiwa na sisi, hutufanya tujisikie kuvutiwa nae na kutamani kutumia muda mwingi nae. Tunajisikia kuchoka tunapompenda asiyeonesha kutupenda. Kwa hiyo mtu humpenda zaidi yule anayempenda na yeye.
- Watu unaofanana nao imani, mitazamo na misimamo hupendana zaidi kuliko wale wanaotofautiana imani, mitazamo na misimamo. Kufanana kunakoambatana na mvuto wa kimwili, huchochea mvuto, na mvuto huo huchochea kufanana. Hata hivyo, watafiti wanasema, zipo tofauti za kihaiba ambazo kwa kawaida huchochea kuvutiana. Mfano mtu mzungumzaji hujisikia kuvutiwa (reinforced) na mtu anayeweza kumsikiliza na si yule anayetaka kuzungumza kama yeye.
- Kumwamini unayevutiwa naye, humfanya avutike kwako. Hii hutegemea kiwango cha usalama wa kihisia (emotional security) unachokuwa nacho wewe na kiwango hicho hicho cha usalama anachokuwa nacho yeye. Kutokuwa salama kihisia (insecure) kunamaanisha ama kutokujiamini, kutokuamini wengine au vyote viwili, ambavyo huathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano. Unaweza kusoma zaidi kwenye makala haya yaliyopita. Lakini kwa kifupi, nafsi isiyosalama, hushindwa kuamini na hivyo hupunguza kumvutia mwingine.
Jawabu ni ndio. Tafiti zinathibitisha kuwa inawezekana kuhusiana na mtu yeyote anayeweza kukufanya ukajisikia kupata mahitaji yako ya kihisia na kukusababisha na wewe uweze kutambua na kujibu mahitaji yake ya kihisia kama tulivyoona kwenye makala zilizopita. Kwa muhtasari tu, tunazungumzia namna gani mwanaume anamfanya mwanamke ajisikie kupendwa, na hivyo kuwa na hamasa ya kumfanya mwanamke huyo amfanye mwanaume husika ajisikie mwenye mamlaka.
Kama tulivyoona awali, ukaribu na mtu hata asiyekuvutia unaweza kuamsha hisia za kuvutiwa kadri unavyoonana nae na namna mtu huyo anavyoweza kuonekana kuelewa na kujibu mahitaji yako ya kihisia. Tunaambiwa, sura unayoweza kuiita mbaya, inapoambatana na jitihada za kutambua na kuelewa mahitaji yako ya kihisia, mitazamo na imani inayofanana na ya kwako, inayokufanya ujisikie vizuri, basi, hatua kwa hatua 'ubaya' wa sura hiyo uliouona awali, hupotea na kugeuka kuwa uzuri.
Vile vile, namna gani uhusiano unakupa kipimo kinachofanana na kile ulichowekeza kwenye mahusiano na hivyo kujenga hali fulani ya usawa (equity), ndivyo uhusiano huo unavyoimarika na kudumu. Watu hawapendi kuonekana wanagharimika zaidi kwenye mahusiano kuliko huyo wanayehusiana nae. Inawafanya wajisikie kubeba mzigo. Wanashusha ego zao. Ndio maana inapoonekana kuwa huyo unayehusiana naye hana uliochonacho, mara nyingi, humbidi anayepungukiwa kufidia kile asichonacho kwa namna nyingine, ili kumfanya mwenzake ajisikie kuwekeza sambamba na alichowekeza mwenza wake.
Kwa mfano, mwanaume asiye na elimu, anapoanzisha uhusiano na mwanamke anayemzidi kielimu, huweza kujikuta katika mazingira ya kutokujiamini. Ili ajisikie vizuri, yaani ajiamini, kwa kujua au kutokujua mwanamme huwa na kingine kinachofidia tofauti hiyo ya elimu ili kudumisha uhusiano huo. Inaweza kuwa uwezo wa kifedha, umaarufu na kadhalika.
Kwa hiyo tunachokisema ni kwamba, inawezekana kuhusiana na mtu yeyote. Na kwa hakika, si kweli kwamba mahusiano bora huwezekana unapokutana na watu sahihi, right women/men. Kama tulivyoona mahusiano yoyote huanza kwa njia ya nasibu, kutegemeana na uliko na unayeonana nae. Kinachowaunganisha watu wawili kimapenzi ni namna wanavyoweza kuelewa na kuitikia ipasavyo mahitaji yao ya kihisia.
Kwamba, mtu sahihi ni matokeo ya mtazamo, imani na matarajio yako. Mtu sahihi kwenye mahusiano ni wewe na sio huyo unayeonana nae. Kwamba ndio, ukiweza kumnyafanya akufanye ujisikie kupendwa, ni dhahiri unaweza kumpenda na kuishi na mtu yeyote tofauti na wanavyoamini watu wengi.
Katika makala yanayofuata, tutaanza kujadili, kwa nini wapenzi huanza kupishana na hatimaye kuanza kushindwa kuwasiliana ipasavyo na kisha kuingia kwenye migogoro ya kimahusiano.
Leave a Comment