Jando na Unyago:Nini Mbadala Katika Karne Hii ya Utandawazi?





Jando na Unyago ilikuwa ni shule ya malezi bora kwa vijana ambao walikuwa wanahama toka rika ya watoto kuwa watu wazima.

Mafunzo ya jando kwa wavulana yaliendana na kutahiriwa na hata kwa wasichana katika baadhi ya makabila. Makabila maarufu katika utamaduni huu ni Wazaramo,Wamakonde,Wakrya,Wayao na makabila mengi ya mkoa wa Singida.
Vijana waliwapatiwa mafunzo juu ya maadili bora, kuwaheshimu wakubwa, kuwa shupavu, uwajibikaji, majukumu ya kuilinda familia, ukoo na kabila.

Mafunzo ya Maisha kwa Vijana Kupitia Jando na Unyago:

Mafunzo katika jando na unyago yalikuwa na nia ya kumuandaa kijana kuingia katika majukumu ya utu uzima.
Wasichana walifundishwa jinsi ya kutunza nyumba, jinsi ya kutunza watoto,lakini pia lazima tuseme walifundishwa jinsi ya kufanya mapenzi na kumridhisha mume.
Hii ya mwisho inaweza ikahitaji mjadala kidogo kama ni sahihi na tutaijadili hapo baadae.
Kwa msichana ilikuwa ni kawaida kuolewa mara baada ya unyago. Kwa baadhi ya makabila kama wazaramo msichana akishaingia unyagoni hufungiwa ndani hadi siku akipata mume wa kumuoa ndio anatolewa.
Kwa ujumla wake mafunzo haya yalisaidia sana kwa vijana kujitambua na kutambua mabadiliko ya ukuaji wao. Pia elimu hii iliwasaidia kupambana na changamoto za familia na kudumisha amani na upendo ndani ya familia zao. Vitu ambavyo vijana wa leo wanavikosa,au kama wanavipata zinapatikana katika vyanzo visivyo rasmi na vinatofautiana sana kati ya kijana mmoja na mwingine kwa kuwa si rasmi.
jando-na-unyago_mafunzo-maasai
Vijana Wakiwa katika Mafunzo ya Ujasiri na Kujihami Katika Jando
jando-na-unyago_unyago-1
Wasichana wakiwa Wamejifunika Mablanketi wakiwa Unyagoni

 Hali ya Malezi na Mafunzo kwa Vijana Hivi Sasa

Malezi ya vijana katika karne hii ya utandawazi in changamoto nyingi. Vijana wanakosa elimu juu ya ukuaji na mabadiliko ya mwili waoili waweze kujitambua na kuchukua hatua stahili katika maisha.
Pia wanakosa elimu na ustadi wa kukabiliana na maisha kama wazai,kama wake au waume. Vitu ambavyo vilikuwa vikifanyika katika unyago na jando lakini sasa hivi hili halifanyiki kutokana na mila hizi kuachwa kwasababu ya mabadiliko ya mitindo yetu ya maisha inayoletwa na utandawazi.
Utandawazi unatafsiriwa kuwa ni mfumo wa uhisiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi.
Ukiachia faida nyingi ambazo utandawazi umeleta lakini bia kuna mabadiliko hasi kama kutozingatiwa kwa baadhi ya tamaduni zetu za asili ambazo zinafaida sana kama Jando na Unyago.
Sasa swali kubwa ni kuwa je,watoto wetu wanafundishwa na nani na wapi?
Wazazi hawafanyi hivyo kwa kuamini kuwa si vyema kwa mzazi kumfundisha mtoto wake elimu juu ya ukuaji na mabadiliko ya mwili kama kubarehe na kuvunja ungo na elimu ya kujamiiana.
Hapo awali vijana walikuwa wakifundwa katika unyago na jando na makungwi walikuwa wakufunzi juu ya mambo haya na walikuwa na jukumu la kufanya haya kwa niaba ya wazazi na jamii husika.
Lakini sasa hivi kungwi wa watoto wetu ni nani? Mitandao ya kijamii kama FaceBook ,twitter na WhatApp? TV na Video wanazoanfgalia usiku na mchana pengine hata bila mipaka? Je teknolojia hizi zinatoa mafunzo yanayotakikana katika jamii zetu? Haya yote ni maswali ambayo yanahitaji majibu na hatua za haraka.

Tunahitaji Jando na Unyago Mamboleo

Ili kuepusha kizazi chetu na balaa la kuwa na familia zisizo na maadili na mbinu za maisha ni budi kurudisha mfumo wa Jando na Unyago.
Kuna mambo ambayo katika mafunzo ya zamani hayakuchukuliwa kuwa na faida katika maisha ya leo ya sayansi na teknolojia,japo yalikuwa na maana katika wakati ule.
Baadhi ya mambo yanayohitaji kubadilishwa na kuachwa ni kama Ktahiriwa kwa wasichana,na elimu ya mapenzi katika umri mdogo.
Tuunde mfumo mpya mabao utabakiza baadhi ya mafunzo katika mfumo ule wa zamani na kuongeza vtu vipya ambavyo vinaendana na karne hii.

Vitu vya kubakizwa:

  1. Mafunzo juu ya kuishi kama baba au mama,mume au mke
  2. Mafunzo juu ya kulinda,kuitunza na kuijali familia
  3. Mafunzo juu ya mabadiliko ya kibayolojia kwa vijana na hatua za kuchukua na wakati muafaka wa kuchukua hatua hizo
  4. Uzalendo kwa familia,ukoo,kabila na taifa

Mambo ya kuondoa:

  1. Vitendo vinavyonyanyasa wanawake kijinsia kama tohara
  2. Kutoa mafundisho kwa watoto ambao hawajafikia umri unaofaa
  3. Kufungia wasichana ndani kwa muda mrefu mpaka wapate mchumba
Mambo mapya yakuongeza ili kuboresha:
  1. Kugawa mafunzo katika awamu mbili:
Mafunzo yafanyike wakati wa vijana kubalehe na kabla hawajaingia katika ndoa-Hii itasaidia kutofautisha mafunzo katika rika hizi mbili. Zamani vijana walikuwa wanaoa na kuolewa wakiwa wadogo sana tofauti na sasa ambapo wengi wanaoa au kuolewa wakiwa naumri kati ya 25-35
  1. Kurasmisha mfumo huu wa mafunzo ya ukuaji kwa vijana katika mitaala ya elimu:
Vijana waende katika mafunzo rasmi kama ilivyokatika mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa(JKT).
  1. Kuingiza mafunzo ya ukuaji na maisha katika shule za awali(Shule za msingi na sekondari)
Kwa kuzingatia haya tutakuwa na mfumo ulioboreshwa wa kuto mafunzo kwa vijana ambao wanajenda familia na taifa la kesho.
Tukumbuke,wabakaji,majambazi na mafisadi wanatoka majumbani kwetu na katika familia zetu. Kama vijana wakikuzwa katika maadili yaliyo mazuri na yanayoklubalika kitaifa basi ni wazi tutajenga taifa lenye watu wanaowajibika , wachapakazi na wazalendo.
Jando na Unyago Mamboleo inaweza ikaleta mapinduzi makubwa katika malezi kwa vijana katika karne hii ya utandawazi.
Je una maoni juu ya mada hii,hii tafadhari andika hapo chini katika kisanduku cha maoni na utume na ushiriki katika kuleta mabadiliko.

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.