TAARIFA YA HABARI YA LEO JANUARY 18 PLANET FM HII HAPA
18.01.2014 SAA 1:00 USIKU UTAFITI
MWANZA
Utafiti
uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), umebaini kuwa
jamii bado inaficha kesi za ukatili kutokana na mila na desturi za Waafrika
zilizojengeka miongoni mwao.
Utafiti huo
umebainishwa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Bukoli iliyoko mkoani hapo,
Christian Mwalimu, ambapo amesema kesi nyingi za kutelekeza familia, vipigo na
unyanyasaji kwa wanawake, hukosa ushahidi kutokana na mlalamikaji kupewa
vitisho vya maisha yake.
Amesema kuwa
wanapokea kesi nyingi za ukatili wa kijinsia, hasa za manyanyaso ndani ya ndoa
kwa mwanamke, kesi ambazo mara nyingi hazitolewi hukumu kutokana na mlalamikaji
kushindwa kutoa ushirikiano na mahakama.
Aidha amesema,
mila ni tatizo kubwa, kwakuwa wanawake waliumbwa kuwa wavumilivu hivyo kutokana
na mila hizo wanalazimishwa kuishi kwa uvumilivu katika ndoa zao.
MWISHO
18.01.2014 SAA 1:00 USIKU UKAGUZI
DODOMA
Waziri
mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Mizengo Pinda amesema ameridhishwa
na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye maeneo mbalimbali ya jengo la Bunge
ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya Bunge lijalo la Katiba mpya.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo asubuhi wakati akipokea maelezo ya ukarabati kutoka
kwa Mhandisi Mkuu wa Ofisi ya Bunge, Eng. Dk. Philemon Mzee, ambaye alikuwa
akimtembeza kwenye maeneo mbalimbali yanayofanyiwa ukarabati ndani ya jengo
hilo.
Dk.
Mzee amemweleza Waziri Mkuu kwamba wanatarajia kuweka viti 670 vya wajumbe wa
kawaida pamoja na viti 24 kwa ajili ya wajumbe wenye mahitaji maalum kama ya
walemavu na mengineyo.
Katika
ukumbi huo viti vya Spika na Makatibu wa Bunge pamoja na mfumo wa vipaza sauti umekamilika
na kwamba kila kipaza sauti kimoja kitakuwa kinatumiwa na watu wawili kulingana
na mpangilio wa ukaaji ulivyo hivi sasa.
Kwa
mujibu wa Dk. Mzee, ukarabati huo unatarajiwa kukamilika Januari 30, mwaka huu
ili kuweza kufanikisha zoezi zima la bunge la katiba kwenda kama ilivyo
kusudiwa.
MWISHO
18.01.2014 SAA 1:00 USIKU USHIRIKIANO
DAR-ES-ASALAAM
Serikali
ya Tanzania imedhamiria kuimarisha ushirikiano baina yake na nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Nyanja mbali mbali za miundombinu.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samuel Sitta wakati
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Mh.Sitta
amebainisha kuwa mwishoni mwa mwaka 2013, Mawaziri wa Tanzania, Burundi, na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walikutana kujadili namna ya kuimarisha miundo
mbinu ya barabara, reli,anga na maji.
Aliongeza
kuwa katika kikao hicho ilikubaliwa kuwa, Shirikika la ndege la Tanzania (ATCL)
lipanue huduma zake na kufika nchini Burundi ambapo lilianza kufanya safari
zake kati ya Tanzania na Burundi Desemba16, mwaka jana mara tatu kwa wiki, kama
hatua za awali za utekelezaji.
Aidha
katika mkutano wa 8 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo, umeridhia mfumo wa
himaya moja ya Forodha na mpangokazi unaoainisha masuala ya utekelezaji katika
kipindi cha miezi sita, ili kuwezesha kuanzishwa kwa himaya ifikapo Juni 2014.
MWISHO
18.01.2014 SAA 1:00 USIKU VIFO
CAIRO
Waziri wa
afya nchini Misri amesema kuwa, idadi ya watu waliofariki katika ghasia za
kisiasa wakati kura ya maamuzi kuhusu katiba mpya ilipokuwa inaendelea imefikia
watu 4 huku wengine 15 kujeruhiwa siku ya jana.
Ghasia hizo
zilianza baada ya wafuasi wa aliyekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi kuandamana
mjini Cairo, na katika mikoa mingine wakiilaani rasimu ya katiba inayopigiwa
kura nchini humo.
Polisi nchini
humo walilazimika kufyatua gesi ya kutoa machozi hewani ili kuwatawanya
waandamanaji hao, ambao hawakuwa na kibali cha kuwaruhusu kufanya maandamano.
Tangu
mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa mamlakani Mohammed Morsi mwezi Julai mwaka
jana, wanaharakati wa vuguvugu la Muslim Brotherhood, wamekuwa wakifanya vurugu
kuipinga serikali ya mpito wakisema kuwa sio ya halali.
MWISHO
18.01.2014 SAA 1:00 USIKU SHAMBULIZI
KABUL
Watu 16 wameuawa wakiwemo wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa,
katika mlipuko wa bomu na shambulizi la risasi lililofanywa kwenye hoteli moja nchini
Afghanistan.
Taarifa zinasema kuwa mlipuaji wa kujitoa
mhanga amejilipua nje ya mgahawa uliokuwa umejaa raia wa kigeni na wa Afghanstan,
wakati watu wengine wawili waliokuwa na bunduki waliingia ndani na kuanza
kufyatua risasi kiholela.
Mkuu wa polisi mjini Kabul, Jenerali Mohammad
Zahir amesema watu 16 waliouawa wote walikuwa ndani ya mgahawa huo ambapo raia
wa kigeni na wa Afghan ni miongoni mwa waliouawa.
Aidha katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki
Moon amethibitisha na kusema kuwa, mwakilishi wa Shirika la Fedha Ulimwenguni –
IMF nchini Afghanistan Bw.Wabel
Abdallah, ni miongoni mwa waliouawa
Katibu mkuu huyo amelaani vikali shambulizi
hilo akisema mashambulizi ya aina hiyo yanayowalenga raia kamwe hayawezi
kukubalika na yanakiuka sheria za kimataifa.
MWISHO
18.01.2014 SAA 1:00 USIKU MAZUNGUMZO
MOSCOW
Matayarisho ya mkutano wa wiki ijayo kusaka
amani nchini Syria, yanaelezwa kufikia hatua nzuri, ambapo Waziri wa Mambo ya
Nje Walid Mualle ametangaza mpango wa kubadilishana wafungwa na waasi wa nchi
hiyo.
Muallem
amesema, ameikabidhi serikali ya Urusi mipango ya usitishaji mapigano katika
mji mkubwa zaidi wa Aleppo, na kwamba serikali yake iko tayari kubadilishana
orodha na makundi ya waasi juu ya uwezekano wa kubadilishana kwa wafungwa.
Suala muhimu
katika matayarisho ya mkutano huo, limekuwa ushiriki wa Iran, ambapo Urusi inataka
Iran iwemo kwenye mazungumzo, huku mataifa ya Magharibi yakiishutumu nchi hiyo
kuusaidia utawala wa Assad na makundi
yake.
Aidha makundi
ya upinzani ya nchini Syria, ambayo yamekuwa yakishindwa kuwa na msimamo wa
pamoja, yanakutana leo mjini Istanbul, Uturuki, kuamua ikiwa yashiriki au yasishiriki
kwenye mazungumzo hayo ya amani yanayoihusu nchi ya Syria.
MWISHO
Leave a Comment