Algeria yaanza siku 3 za maombolezi
Mabaki ya ndege ya jeshi la Algeria iliyoanguka hapo jana.
Algeria imeanza siku tatu za
maombolezi ya kitaifa kufuatia ajali ya ndege iliyowaua watu sabini na
saba Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Abiria mmoja alinusurika ajali hiyo iliyohusisha
ndege aina ya Hercules C-130 iliyoanguka katika eneo la milima ya Oum
al-Bouaghi, ikiwa njiani kuelekea mji wa Constantine.
Ripoti zinasema hali mbaya ya anga ilisababisha ajali hiyo ya ndege.
Rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika amewasifu wanajeshi waliopoteza maisha yao na kuwataja kama wafia dini wa taifa hilo.
Wengi wa abiria sabini na nane waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni maafisa wa kijeshi na familia zao.
Mwanajeshi aliyenusurika, anaripotiwa kuendelea
kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Constantine baada ya kupata
majeraha ya kichwa.
Wizara ya Ulinzi imesema kuwa imeunda tume
maalum kuchunguza ajali hiyo na kuwa Ahmed Gaid Salah, ambaye ni mkuu wa
majeshi na naibu waziri wa Ulinzi atazuru eneo la ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya
habari, wizara ya ulinzi imesema kuwa hali mbaya ya anga iliyohusisha
kimbunga na mvua kubwa ya barafu ilisababisha ajali hiyo.
Runinga ya taifa ilionyesha picha za ajali hiyo.
Awali maafisa wa Ulinzi na shirika hilo la
habari waliripoti kuwa watu 103 walikuwa ndani ya ndege hiyo lakini
idadi hiyo ilipunguzwa hadi watu sabini na nane.
Leave a Comment