Ijue maana ya neno TANZANIA, lilipotokea na aliyelibuni
Leo tunasherehekea miaka 50 ya
Muungano,ikumbukwe pia kwamba unapotaja historia ya muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ni dhahiri kwamba hutaacha kutaja majina ya
wapigania uhuru na viongozi mbalimbali walioiongoza tangu enzi za
ukoloni, hadi kupata uhuru.
Hata hivyo, katika kila historia ya
taifa lolote iliyojengwa, kuna watu waliofanikisha historia hiyo, lakini
kwa sababu moja au nyingine, michango ya baadhi yao imesahaulika na
pengine kutotajwa kabisa kwenye historia hizo.
Wengi wa Watanzania tunafahamu kuwa jina la nchi yetu Tanzania, limetokana na majina ya nchi mbili
zilizoungana na kuwa moja ambazo ni Tanganyika na Zanzibar. Hivi ndivyo
tulivyofundishwa shuleni. Wengine wanaamini kuwa Rais wa kwanza na
muasisi wa taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyebuni
jina la Tanzania.
Lakini ukweli ni kwamba, jina la
Tanzania lilibuniwa na mmoja wa wananchi walioshiriki mchakato wa
kutafuta jina la nchi hii, baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar
mwaka 1964.
Mohammed Iqbal Dar ndiye aliyebuni jina la Tanzania, wakati huo akiwa na umri wa miaka 18 akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe.
Ilikuwaje sasa?
“Nilikuwa maktaba najisomea, nilishika gazeti la Daily News, wakati huo likiitwa The Standard, ndipo nikaona tangazo hilo,” anaeleza Mohammed Iqbal Dar alivyopata hamasa na kuongeza:
“Siku
hiyo hiyo, nikafanya majaribio ya kutafuta jina bila hata ya
kuishirikisha familia yangu. Nilichukua karatasi na kalamu, lakini kabla
sijaanza kufanya chochote, nilimwomba Mungu aniwezeshe kwa maana
naamini Mungu, ndiye kila kitu wakati wa kufanya jambo lolote.”
“Kwa hiyo kwenye ile karatasi nikaandika Tanganyika na Zanzibar kisha, nikaandika majina yangu mawili; Iqbal na Ahmadiya,” anasema Dar na kufafanua kuwa Iqbal ni jina lake na jina la ubini na Ahmadiyya ndiyo dhehebu lake.
Kupata jina Tanzania:
Akisimulia alivyopata jina Tanzania, anasema kuwa ilimchukua dakika tano tu kufikiria na kulipata jina hilo.
“Nilichukua Tan kutoka kwenye Tanganyika na kuongeza Zan kutoka kwenye Zanzibar na kupata Tanzan, niliona halitimii vizuri,”anasimulia Dar.
Anabainisha kuwa baadaye alifikiria na
kugundua kuwa majina mengi ya nchi za Afrika yanaishia na IA mfano
akitoa mfano wa Ethiopia, Gambia, Tunisia, Nigeria, Algeria, Somalia,
Zambia, Namibia na kwamba baada ya kubaini hilo aliamua kuongezea herufi
hizo mbili na kupata jina Tanzania.
“Nilituma maombi yangu katika shindano hilo, bila kumwambia mtu yeyote nyumbani,” anasema Dar.
Baada ya muda mfupi baba yake, mzee
Tufail Ahmad Dar, alipokea barua kutoka Wizara ya Habari na Utalii
(wakati huo), ambapo ndani yake kulikuwa na ujumbe wa pongezi ya kwamba
kijana wake ameshinda katika shindano hilo.
“Wakati
naandika, sikuwa na matumaini kama nitashinda kwa kuwa shindano hilo
lilikua wazi kwa watu mbalimbali, hivyo sikuwa na tarajio lolote kama
ningeshinda,
“Jioni wakati narudi nyumbani,
baba mzazi alinifungulia mlango wakati si kawaida yake kwani mama ndiye
alikuwa akinifungulia siku zote, hapo nikajua kuna kitu hakipo sawa.
Lakini, nilikaribishwa na tabasamu la baba, pamoja na pongezi nyingi,
nilifurahi sana,” anaeleza.
Tuzo:
Dar anasema kuwa kwa ushindi huo, alitunukiwa ngao pamoja na fedha taslimu Sh200 kama zawadi ya ubunifu wake.
Pamoja na kuibuka mshindi wa ubunifu huo
na hadi leo jina la Tanzania alilolibuni yeye linaendelea kutumika,
lakini Dar anadai kuwa mchango wake huo kwa taifa ni kama hautambuliwi
na Serikali imemsahau katika kuandika historia ya taifa la Tanzania.
“Sijui kwa nini sitambuliwi tangu
wakati huo? Hakuna chochote kinachoelezea uhusika wangu katika kupata
jina la Tanzania na ukiwauliza watu, wengi watakwambia ilikuwa ni
Nyerere aliyeleta jina Tanzania, hii inaumiza,” anasema akilalamika.
Mohammed Iqbal Dar alizaliwa mwaka 1944 jijini Tanga, ni mtoto wa tatu kati ya watoto saba wa Tufail Ahmad Dar. Dar
ni baba wa mtoto mmoja, ambapo kwa zaidi ya miaka 40 sasa amekuwa
akiishi nchini Uingereza alikoenda kwa ajili ya kusoma kabla ya kuwa
raia wa nchi hiyo.
Mbunifu huyo wa jina la Tanzania ni
Mhandisi wa Masuala ya Redio, kazi anayoifanya nchini Uingereza,
akieleza kuwa katika kuienzi nchi yake, nyumba yake iliyopo mjini
Birmingham, ameipa jina la Dar es Salaam, ikiwakilisha ubini wake,
pamoja na Jiji la Dar es Salaam.
Leave a Comment