VYANZO VYA MAJI VYA MAPOROMOKO VILINDWE
SERIKALI imeshauriwa
kulinda vyanzo vya maji vya asili vinavyotokana na maporomoko ya maji vinavyosaidia
uzalishaji wa Nishati ya Umeme, hususani vilivyopo katika Bwawa la Kidatu na
Mtera, ili
kuepusha uanzishwa au matumizi ya vyanzo vingine vinavyochangia ongezeko la uzalishaji
wa hewa ukaa na gesi joto kwa wingi duniani na hata kuharibu Tabaka la Ozoni (Ozone
layer).
Ushauri huo ulitolewa na Meneja Uhifadhi wa Mfuko wa
Uhifadhi wa mazingira duniani (WWF), upande wa Tanzania, Gerald Kamwenda,
wakati akizungumza na wadau wa nishati na mazingira wanaokutana mjini Morogoro,
ambapo alisema hewa ukaa na gesi joto, vimekuwa vikisababisha mabadiliko ya
tabia nchini ikiwemo kuongezeka kwa joto la dunia, lakini dunia itaweza kuokolewa
iwapo jitihada zitaongezwa kwa kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kutumia
nishati Jadilifu kwa matumizi ya kila siku.
Alisema nishati jadilifu zinaweza kupatikana
kutokana na mazingira mbalimbali kama upepo, kinyesi cha wanyama na umeme wa
maji, ambao umekuwa ukisaidia kupatikana kwa nishati safi isiyo na athari
kimatumizi, tofauti na umeme wa mafuta, ambao nguvu zake zimeendelea kuelekezwa
na Serikali katika maeneo kama ya Kinyerezi, ambao huchangia uzalishaji wa gesi
joto duniani.
Alibainisha
kuwa Hewa ya ukaa inayotokana na mafuta ni mbaya zaidi
ikilinganishwa na ile inayotokana na gesi, kwahiyo ni vyema Serikali
ikaendelea kutilia nguvu katika utunzaji wa vyanzo vya maji vya mabwawa
ya Kidatu na Mtera
ambayo ni vyanzo vya asili, ingawa kwa kiasi Fulani vyanzo vinavyopeleka
maji
katika mabwawa hayo vinaathiriwa na mpango wa kilimo kwanza, kwa
wananchi
jirani na mito kama Ruaha uliotegemewa kutiririsha maji mwaka
mzima,kuziba maji
hayo badala yake kuyaelekeza yasaidia kilimo kwa njia zisizo endelevu.
Alisema baadhi ya nchi dunia zimeweza kupiga hatua
katika matumizi ya Nishati Jadilifu, na kwamba hata kwa Tanzania itawezekana
iwapo kila mdau zikiwemo asasi za kiraia na Taasisi za Kiserikali,
watashirikiana kubaini mambo mbalimbali yakayosaidia kukabiliana na uharibifu
wa mazingira, gharama nafuu ya vifaa na miundo mbinu ya nishati jadilifu kama
nishati ya jua, nishati ya upepo, nishati ya maji na nishati ya kinyesi
(mbolea).
“Kwa kutumia nishati Jadilifu, inasaidia pia
kutekeleza nguzo kuu tatu za MKUKUTA yaani kukuza uchumi na kupunguza umaskini,
ustawi wa jamii na maisha bora kwa kila Mtanzania na hata suala zima la Utawala
Bora”Aliongeza Meneja huyo wa Uhifadhi wa WWF.
Kwa upande wao Meneja Mradi wa Mafuta (Oil Project)
wa WWF, Theresia Ole Mako, na Afisa Programu wa WWF Tanzania, Novat
Kessy,walibainisha mfuko huo umebuni mradi utakaotekelezwa kwa kipindi cha
miaka mitatu kuanzia 2014 hadi 2016, ukilenga kuangalia kanda ya Afrika, ili
kuhakikisha nishati Jadilifu inafikiwa na watu wengi.
Ole Mako alishauri uwepo wa madawati ya Nishati hadi
katika ngazi ya wilaya kama ilivyo kwenye maeneo mengine kama Kilimo,
Maliasili, Ufugaji, Michezo na Utamaduni, badala ya suala hilo kubaki makao
makuu pekee, ili kusaidia utekelezaji na usimamizi mzuri wa sera zinazohusu
masuala ya Nishati na Mazingira.
Alisema nia ya mradi huo ni kuhakikisha asasi za
kijamii zinaweza kuwafikia wanaotumia nishati hiyo, kwa kuangalia nishati
zinazotumika katika maeneo husika, fursa rahisi zilizopo katika maeneo
mbalimbali kama upepo, jua, vinyesi vya wanyama na fursa nyingine, na jitihada
zinazofanywa kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na kupunguza mabadiliko ya
hali ya hewa.
Alisisitiza kila mtanzania anapaswa kuhakikisha
mazingira yanakuwa salama hata kwa kizazi kijacho, bila kujali atanufaikaje na
usalama anaoutengeneza sasa, kupunguza matumizi ya mkaa ambayo yameonekana kuwa
makubwa na mkaa kuvunwa kwa wingi kuliko unavyohifadhiwa, namna gani mtanzania
hata wa hali ya chini ataweza kupata vifaa vya matumizi ya nishati jadidifu kwa
matumizi ya kawaida.
Alizishauri Asasi za Kiraia kushirikiana na taasisi za
Kiserikali ili kuwa na namna bora ya kufikia malengo ya pamoja hasa katika matumizi endelevu ya nishati Jadidifu.
Leave a Comment