WATANZANIA leo wanaelekeza
macho na masikio yao mjini Dodoma, kusikiliza Hotuba ya Bajeti ya
Serikali, inayotarajiwa kusomwa saa 10 kamili bungeni na Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum. Tayari Waziri Saada alishaeleza kuwa makadirio
ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, unaoanza Julai
mwaka huu, yatakuwa Sh trilioni 19.6 kutoka makadirio ya Sh trilioni
18.2 ya Bajeti inayoisha muda wake.
Vipaumbele vya Bajeti hiyo, kwa maana ya
miradi itakayozingatiwa zaidi, ni iliyo katika Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) unaohusisha sekta sita za Kilimo, Elimu, Maji,
Utafutaji rasilimali fedha, Nishati, Uchukuzi na Uboreshaji wa Mazingira
ya kufanyia biashara na Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano.
Akisoma mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo kwa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano
na Uratibu, Stephen Wassira, alisema mapendekezo ya mpango huo, yana
vipaumbele vitano. Cha kwanza ni miundombinu, kikifuatiwa na kilimo,
viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuongeza thamani, maendeleo
ya rasilimali watu na ujuzi na uendelezaji wa shughuli za utalii,
biashara na fedha.
Katika hotuba hiyo, Watanzania wengi
watakuwa makini kusikiliza bidhaa na huduma zitakazoongezwa kodi, jambo
linalotarajiwa kuongeza bei ya bidhaa za huduma husika katika soko.
Katika bajeti inayoishia, Serikali iliongeza kodi kwenye magari
makuukuu, bia, vinywaji vikali na baridi ambavyo kodi imekuwa ikiongezwa
kila mwaka na kuwaathiri watumiaji.
Kutokana na hali hiyo wanywaji pombe na
sigara baada ya bajeti ya mwaka juzi ya 2012/2013, walilazimika kutumia
fedha nyingi ili kupata huduma hizo kwa kiwango kile kile katika mwaka
huu wa bajeti unaoisha. Bidhaa zisizokuwa za mafuta ambazo zilifanyiwa
marekebisho na kuongezwa kodi ni mvinyo, pombe, vinywaji vikali, na
sigara.
Ushuru pia uliongezwa kwenye magari
yasiyokuwa ya uzalishaji na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20
mpaka asilimia 25. Lengo la Serikali katika hilo, lilikuwa kupunguza
uagizaji wa magari chakavu ili kulinda mazingira na kupunguza ajali za
mara kwa mara. Katika bajeti hiyo, vijana wa bodaboda walicheka baada ya
Serikali kusamehe ushuru wa barabara kwa pikipiki hizo za biashara.
Moja ya kivutio kikubwa cha Bajeti
inayowasilishwa leo, ni matarajio ya wafanyakazi kuhusu utekelezaji wa
ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa katika sherehe za Mei Mosi mwaka
huu, ya kuongeza mshahara wa kima cha chini na kupunguza kodi ya
mshahara (PAYE). Rais Kikwete alisema Serikali itaendelea kuongeza
mshahara wa kima cha chini na kubainisha kuwa mwaka 2005 alipoingia
madarakani, alikuta mshahara wa kima cha chini ni Sh 65,000 na
kukipandisha taratibu hadi kufikia Sh 240,000 cha sasa.
Kuhusu kupunguza PAYE, Rais Kikwete
alisema kusudi la Serikali ni kupunguza kodi hiyo ya mshahara kutoka
asilimia 13 inayotozwa sasa, ifikie katika kiwango cha tarakimu moja.
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo mwaka huu
imekuwa gumzo bungeni, huku wabunge wengi wakitaka ipunguzwe, Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alinukuliwa akisema wafanyabiashara na
vigogo wanaokwepa kodi kwa kujificha kwenye mwavuli wa misahama, hawako
salama.
“Tutafuatilia kikamilifu kwa kuwa wapo
watu wanaingiza bidhaa wanapewa msamaha, lakini ukija kwenye huduma za
jamii unakuta bidhaa hizo zinauzwa kibiashara,” alisema. Mwigulu pia
alizungumzia ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya fedha za Serikali na
kufafanua kuwa, yatadhibitiwa.
“Bahati nzuri niliyonayo, sikuzaliwa na
chembe ya woga, kwa hiyo kwenye hili hakuna mkubwa wala mdogo, hakuna
mtu atagusa fedha ya umma kwa kukwepa au kwa kutumia vibaya kodi ambayo
ilishakusanywa halafu akapona asiguswe,” alisema.
Mwigulu alisema katika Bajeti ya
Serikali ya 2014/2015, yapo mambo ya msingi matano, ambayo yatasimamiwa
kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa tofauti na
zilizopita. Mbali na kuondoa misamaha ya kodi, pia makusanyo ya ndani
yatatiliwa mkazo zaidi ili kujenga uwezo wa kujitegemea wenyewe badala
ya kutegemea wahisani.
Jambo la tatu alisema ni kuhakikisha
Serikali inapeleka fedha kwenye mahitaji muhimu na kwa wakati, ili fedha
za maendeleo zitumike kama ilivyokusudiwa. Jambo la nne
litakalozingatiwa kwa mujibu wa Mwigulu, ni usimamizi wa fedha
zinazopatikana kwani pamoja na makusanyo kidogo, lakini pia kuna
uvujaji. “Tunataka fedha inayopatikana na kupangiwa kazi fulani itumike
kwa shughuli iliyokusudiwa. Tutahakikisha tunasimamia na kudhibiti
matumizi yake,” alisema.
Naibu Waziri huyo wa Fedha alisema eneo
la tano ambalo litaangaliwa ni fedha ambazo hazitokani na kodi, bali
zinachangwa na wananchi na wadau wengine katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo. Alisema eneo hilo ni muhimu mbalo Serikali inaona kuna haja
ya kulisimamia vizuri, ili kuhakikisha fedha za wananchi zinatumika
vizuri. Kwa upande wa Kenya, hotuba ya Bajeti ya Serikali ya Kenya,
itasomwa na Waziri wa Fedha, Henry Rotich.
Katika taarifa yake kwa wabunge wa Kenya
mwezi Machi mwaka huu, Rotich alieleza kuwa Bajeti ya Kenya kwa mwaka
wa Fedha wa 2014/15, itakuwa Shilingi za Kenya Trilioni 1.8. Waziri wa
Fedha wa Uganda, Maria Kiwanuka ndiye atakayesoma hotuba ya Bajeti ya
Serikali ya Uganda kwa mwaka wa fedha 2014/15. Kiwanuka ataeleza hatua
mbalimbali za kuinua uchumi, kupunguza kodi mbalimbali na kudhibiti
mfumko wa bei. Hivi karibuni, Kiwanuka alikaririwa akisema kuwa uchumi
wa Uganda unaendelea kukua kwa kasi, lakini siyo katika viwango vya
miaka 1990 na 2000, ambapo ulikua kwa asilimia 7.
Kwa upande wa Rwanda, hotuba ya Bajeti
ya Serikali itasomwa na Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda,
Claver Gatete. Bajeti yote ya Rwanda kwa mwaka 2014/15 inatarajia kuwa
Faranga za Rwanda bilioni 1,753. Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani
(IMF), uchumi wa Rwanda unatarajia kukua kwa asilimia 6 katika mwaka wa
fedha 2014/15, ukilinganisha na asilimia 4.6 mwaka 2013.
Waziri wa Fedha, Mipango ya Uchumi na
Maendeleo wa Burundi, Tabu Abdallah Manirakiza, ndiye atasoma bajeti ya
Serikali ya Burundi kwa mwaka wa fedha 2014/15. Tayari Shirika la Fedha
Duniani (IMF) limekadiria kuwa uchumi wa Burundi, utakua kwa asilimia 7
katika mwaka 2014/15, ukilinganisha na asilimia 4.5 mwaka 2013.
|
Leave a Comment