NEYMAR AMWAGA `CHOZI` TENA, ZUNIGA AMPIGIA MAGOTI, NAYE WAKALA WAKE AONJA JEURI YA BWANA MDOGO!
Hisia: Neymar alimwaga machozi, huku
akiweka wazi kuwa alikaribia kuwa kichaa baada ya Juan Zuniga kumfanyia
faulo mbaya kwenye mchezo wa robo fainali ya kombe la dunia dhidi ya
Colombia.
NYOTA wa Brazil, Neymar Jr amefichua
siri kuwa alishindwa kuzuia machozi na alikaribia kuwa kichaa baada ya
kugongwa na Juan Zuniga na kuvunjika mfupa wa uti wa mgongo.
Neymar kwa mara ya kwanza alifanya
mkutano na waandishi wa habari baada ya kutoka Hospitalini ambapo
anauguza majeraha yake ya mfupa wa uti wa mgongo uliovunjika kwenye
mechi ya robo fainali ya kombe la dunia dhidi ya Colombia.
Pia Neymar hajakubaliana na maneno ya
wakala wake aliyemuita Luiz Felipe Scolari kuwa ni kocha mbaya, mwenye
majivuno na aliyepitwa na wakati.
Hii inatokana na kitendo cha Brazil
kufungwa mabao 7-1 dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa nusu fainali ya
kombe la dunia, jumanne ya wiki hii.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 22
ameweka wazi kuwa beki wa Colombia, Juan Zuniga ambaye alimgonga na goti
kwenye uti wa mgongo alimpigia simu na kuomba radhi kwa kitendo hicho
kilichomfanya asicheze tena michuano hii mikubwa duniani.
Neymar jana alitembelea kambi ya mazoezi ya timu ya Taifa ya Brazil iliyopo mjini Teresopolis na aliwasalimia wachezaji wenzake.
Pia ataambatana na wenzake hapo kesho katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu dhidi ya timu ya taifa ya Uholanzi.
Jumapili katika dimba la Maracana, mjini Rio di Janeiro, Argentina itacheza mechi ya fainali dhidi ya Ujerumani.
Machozi: Neymar alishindwa kuendelea kucheza fainali za kombe la dunia baada ya kuvunjika mfupa wa uti wa mgongo.
Kwaheri: Neymar aliweza kutabasamu wakati akiondoka kwenye mkutano wa kwanza na waandishi wa Brazil tangu apate majeruhi.
Amani: Neymar alikiri kuwa Zuniga
amempigia simu na kumuomba radhi kwa kitendo alichomfanyia na kumaliza
ndoto zake za kucheza kombe la dunia
Leave a Comment