Serikali ya shirikisho ya Somalia yakosolewa juu ya namna inavyoshughulikia siasa za dola ya Kusini Magharibi
Wasiwasi kati ya vikundi viwili vyenye siasa tofauti huko Baidoa,
vinavyoongozwa na Mohamed Haji Abdinur na Madobe Nunow Mohamed,
vimefikia hatua mpya baada ya serikali ya Somalia kutangaza mpangilio wa
makubaliano baina ya pande mbili hizo katika mkutano ambao Mohamed
hakuwepo.
Askari wa Ethiopia wanaohudumia chini ya
Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) wakitembea kuelekea
Baidoa, Somalia, tarehe 22 Juni wakati wa kupiga doria katika jiji hilo.
[AMISOM Photo / Tobin Jones]
Abdinur na Mohamed wamekuwa katika kutoelewana juu ya uundaji wa Dola
mpya ya Kusini Magharibi ya Somalia tangia Machi, wakati wawili hao
walipochaguliwa kuwa marais kutokana na pande mbili zenye ushindani huko
Baidoa, moja ikiwa na mamlaka ya dola tatu Bay, Bakol na Shabelle ya
chini, na nyingine ikitoa mwito wa dola mpya inayojumuisha pia Gedo,
Jubba ya chini na Jubba ya kati, ambazo zilizungana kuunda Utawala wa
Muda wa Jubba (IJA) mwaka uliopita.
Lakini tarehe 23 Juni, Serikali ya Somalia ilitangaza kwamba rais wa
dola ya mikoa mitatu, Abdinur, na wawakilishi kutoka dola pinzani za
mikoa sita inayoongozwa na Mohamed walifikia muafaka na kutia saini
makataba huko Mogadishu kuunda kwa pamoja utawala wa muda wa mkoa ikiwa
na mamlaka ya kisheria juu ya Bay, Bakol na Shabelle ya chini.
Hatahivyo Mohamed, alitupilia mbali mkataba huo, akiuita "batili" kwa
sababu waziri aliyeutia saini kwa niaba yake, Abdifatah Mohamed Ibrahim,
hakumwakilisha na alishaondolewa kwenye majukumu yake kabla ya
kushiriki katika majadiliano hayo.
Mazungumzo zaidi, usuluhishi unahitajika
Mkataba huo umekumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa viongozi wa koo na
wanasiasa ambao walitoa wito kwa serikali ya shirikisho kutangua mkataba
huo na kuwezesha mazungumzo zaidi kuhakikisha ushiriki wa wadau wote
katika mchakato wa usuluhishi.
Raia pia walipinga makubaliano, wakiwa na siku tatu mfululizo za
maandamano ya umma huko Baidoa ambayo yalimalizika kwa kuanza kwa
Ramadan tarehe 29 Juni.
"Uamuzi wa serikali [kutambua dola tatu za kanda] hautafanya kazi kwa
sababu ni kinyume cha katiba," alisema Hassan Elmi Yahya, mmoja wa wazee
wa ukoo wa Hawiye. "Katiba inaeleza kwamba mikoa miwili au zaidi ambayo
iko katika makubaliano inaweza kuanzisha dola ya shirikiso, lakini watu
wa Shabelle ya Chini hawako tayari kujiunga na Bay na Bakol."
"Kuna vita vya [ukoo] vinavyoendelea katika Shabelle ya Chini. Inahitaji
usuluhishi, kwa hiyo, watu lazima kwanza wapatane," aliiambia Sabahi.
Kwa upande wake, Mohamed, rais wa dola sita za kanda, alisema suala kuu
lililopo ni namna ya kuhakikisha kwamba watu kutoka katika koo zote
ambao wanatoka katika kanda sita zinazohusika wanaweza kushiriki katika
siasa na wanawakilishwa katika serikali zao za mitaa.
Kabla ya kufikia mafikiano, alisema, mazungumzo zaidi yanatakiwa na IJA.
"Hii inaweza kusababisha makubaliano ya namna ya kubainisha [na kulinda
haki za] watu wanaoishi Jubba ambao tunashirikiana jadi zetu na watu
kutoka Jubba wanaoishi Bay, Bakol na Shabelle ya Chini," Mohamed
aliiambia Sabahi.
Makubaliano yaonyesha kutoafikiana katika serikali ya shirikisho
Makubaliano ya ubishi pia yamesababisha mgawanyiko ndani ya serikali ya
shirikisho ya Somalia, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani na Mfumo wa
Shirikisho Abdullahi Godah Barre akipinga dhidi ya hatua hiyo, akiiita
kinyume cha katiba na ya haraka.
"Hadi sasa, Baraza la Mawaziri halijakubaliana kuhusu sheria inayoeleza
utaratibu wa kuanzisha uongozi wa mkoa," Barre alisema katika mahojiano
na Idhaa ya BBC Somalia, akiongeza kwamba suala hilo linapaswa kusubiri
hadi serikali itakapofanya uamuzi wa wazi kuhusu mchakato wa kuanzisha
dola ya shirikisho.
Barre pia alisema wizara yake haikuwa imeambiwa kuhusu makubaliano na kwamba makubaliano kama hayo yanadhoofisha kazi ya wizara.
Hata hivyo, Waziri wa Michezo na Vijana Khalid Omar Ali, ambaye alipewa
kazi ya kuongoza mazungumzo kati ya makundi mawili huko Baidoa kwa niaba
ya serikali ya shirikisho, alitupilia mbali ukosoaji wa Barre na
alisema kulikuwa hakuna ugomvi miongoni mwa viongozi katika serikali ya
shirikisho kuhusu jinsi ya kushughulikia hali ya Baidoa.
"Rais, spika wa bunge na waziri mkuu wote walikubali. Uongozi wa nchi
umefikia muafaka kuhusu makubaliano na baraza la mawaziri limeidhinisha.
Wote kwa pamoja wasingeweza kukubaliana katika hilo kama kungekuwa ni
kitu kisichofaa," aliiambia Sabahi.
Kinachotakiwa kufanyika
Mwenyeji wa Baidoa Ibrahim Ali Ahmed, ambaye alifanya kazi kama Mkuu wa
wilaya ya Zaila chini ya utawala wa Mohamed Siad Barre, alisema njia
pekee ambayo serikali ya mikoa hiyo mitatu inaweza kufanikiwa ni kupitia
mazungumzo na usuluhishi zaidi.
"Kwanza wanatakiwa kukaa pamoja na kumridhisha raisi wa mikoa hiyo
mitatu, Madobe Nunow [Mohamed]. Wanatakiwa pia kupatana na umma. Hicho
ndicho kitakacholeta suluhisho," aliiambia Sabahi. "Hakuna jambo jingine
litakalofanya kazi isipokuwa kama litaanzishwa kwa mazungumzo na
usuluhishi."
Ahmed pia aliwaagiza viongozi wa serikali ya mikoa hiyo mitatu
kuhakikisha koo zinazodharaulika zinazoishi katika mikoa hiyo
zinahusishwa katika uundaji wa utawala wa serikali mpya.
Waziri wa Mipango na Ushirikiano wa serikali ya mikoa mitatu Mohamed
Abdullahi Mursal alisema viongozi kutoka katika serikali yake wanapanga
kufanya mazungumzo na koo zote zinazohusika kama sehemu ya makubaliano.
"Matakwa ya Somalia hayaegemei katika migogoro mipya," aliiambia Sabahi.
"Tutampatia kila mmoja katika mkoa fursa ya kuwa sehemu ya utawala.
Tutazungumza na kila mmoja na mlango wa mazungumzo utabaki wazi kwetu."
Mursal alisema wangeimarisha utawala shirikishi kwa watu wote wanaoishi
katika mikoa hiyo mitatu na kwamba muda wa kuchukua mambo kwa nguvu
umepita.
"Tumeibuka kutoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na hatutarejea
nyuma katika hilo. Tunaahidi kuona katika meza ya mazungumzo mtu yeyote
ambaye hatafuti kufaidika kutokana na vita na mtutu wa bunduki,"
alisema.
Leave a Comment