TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TETESI ZA KUWEPO MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA MKOANI KILIMANJARO
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TETESI ZA KUWEPO MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA MKOANI KILIMANJARO
Utangulizi
Mnamo
tarehe 22 Oktoba 2014, Wizara ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ya kuwepo kwa mgonjwa aliyehisiwa kuwa na
dalili za ugonjwa wa Ebola. Mgonjwa huyu mwanaume ana umri wa miaka 37,
na mkazi wa Dar es salaam (Kimara ) ambaye
alikwenda Kilimanjaro tarehe 20 Oktoba 2014 katika kijiji cha Kirua kwa
ajili ya kusalimia ndugu. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali
( 38.2 0c), maumivu ya Misuli, kuchoka na maumivu ya kichwa pamoja na maumivu ya koo na kupoteza hamu ya kula.
Mgonjwa
huyu anatibiwa katika Kituo cha Afya Shirimatunda, Kilimanjaro kuanzia
tarehe 22.10.2014 ambako yupo hapo hadi sasa. Mgonjwa huyu kikazi ni
“Land Surveyor” na hufanya kazi zake nchini na nje ya nchi ikiwemo nchi
ya Senegali. Mnamo siku za karibuni alikwenda nchini Senegali kwa kazi
za mkataba na kurejea nchini mwanzoni wa Oktoba 2014. Hata hivyo,
mgonjwa huyu hakuwa na historia ya kusafiri kwenda nchi zilizoathirika
na ugonjwa wa Ebola yaani Liberia, Guinea au Sierra Leone.
Hatua zinazochukuliwa hadi sasa;
i. Sampuli ya damu ya mgonjwa kwa ajili ya uchunguzi wa Kimaabara ilifanyiwa uchunguzi na kuonekana kuwa na malaria.
Matokeo ya awali dhidi ya magonjwa ya jamii ya ebola yakiwa ni pamoja
na Dengue na Chikungunya yanaonyesha kuwa mgonjwa hakuwa na magonjwa
haya.
ii. Mgonjwa anaendelea kuhudumiwa katika kituo cha Afya cha Shirimatunda.
iii. Wanafamilia wa karibu pia wamechunguzwa na kuonekana kuwa hawana dalili za ugonjwa wa Ebola.
Mwongozo wa utambuzi wa ugonjwa huu (Standard Case Definition) unaeleza kwamba ili mgonjwa aweze kuhisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola anatakiwa akidhi vigezo vifuatavyo:
i. Dalili
za awali ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli,
kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara nyingi dalili hizi
hufuatiwa na kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele vya ngozi, kwa
baadhi ya wagonjwa hutokwa na damu ndani na nje ya mwili
ii. Awe
amesafiri kwenda sehemu zilizothibitishwa kuwa na ugonjwa wa ebola
ndani ya kipindi cha wiki 3 na hizi zikiwemo Guinea, Sierra Leone na
Liberia. Aidha Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshatangaza kutokuwepo
kwa ugonjwa huu nchini Senegali na Nigreia na hivyo kuzitoa nchi hizi
kwenye nchi hatarishi.
iii. Dalili
nyingine ni Kugusa majimaji kutoka kwa mgonjwa, maiti au
mnyama anayehisiwa au kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.
Hitimisho
Wizara
inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa HAKUNA MGONJWA yeyote
aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa
nchini. Mgonjwa huyu kutoka Kilimanjaro hana ugonjwa wa Ebola bali
anatibiwa kama mgonjwa wa MALARIA.
Adiha
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu ila wanatakiwa kuendelea
kuchukua tahadhari za kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa huu ambazo:-
o Kuepuka
kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na
majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili za
ugonjwa wa Ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
o Kuepuka kushughulikia
maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake
watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za Afya kwa ushauri.
Wataalam watasimamia maziko ikiwa itatokea.
o Wananchi
waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu
na kusababisha kuzidi kueneza kwa ugonjwa wa Ebola.
o Kutoa
taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
o Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu
Imetolewa na,
Dkt. Donan Mmbando
KAIMU KATIBU MKUU
24 Oktoba, 2014
Leave a Comment