Utingo ajaribu kuendesha gari....kilichomkuta ni balaa


Daladala2
Utingo aliyejaribu ku‎endesha daladala amekatisha maisha ya mwanafunzi mmoja na kujeruhi mtu mwingine mmoja, huku wengine wakiponea katika tundu la sindano.
Katika ajali hiyo ya kusikitisha, ndugu wa mwanafunzi huyo aliyefariki wamesimulia kuwa ndugu yao na watu wengine walikuwa wamesimama katika kituo cha mabasi cha Makumbusho ndipo basi hilo lilipokuja na kusimama.
Kwa mujibu wa shuhuda amedai kuwa baada ya dereva kuegesha basi lake na kushuka utingo huyo alijaribu kusogeza gari lakini likamshinda na kujikuta likiwaparamia watu waliokuwa wamesimama kituoni hapo na kupeleka maafa, simanzi, maumivu na mshtuko kwa watu wasiokuwa na hatia.
Imesekana kuwa baada ya ajali hiyo utingo huyo ambaye jina lake halikuweza kujulikana mara moja alifanikiwa kutoroka huku gari hilo lililopelekea ajali hiyo kupelekwa kituo cha polisi cha oysterbay ambako jalada limefunguliwa.
Marehemu wa ajali hiyo ametambuliwa kama Naomi Lawrence Mwalusako, mtoto wa ‎mchezaji maarufu wa zamani wa klabu ya Yanga na Taifa stars ambaye pia ameiongoza Yanga kama Katibu Mkuu.
Cha kusikitisha zaidi ni kuwa marehemu Naomi, ndio alikuwa amemaliza tu mitihani yake ya kidato cha sita huku yeye na familia yake walikuwa na mategemeo na ndoto kubwa kwake.
Zaidi ya marehemu Naomi, mtu mmoja alijeruhiwa sana katika ajali hiyo na hadi sasa amelazwa katika hospitali ya Mwananyamala huku mwili wa Naomi nao ukiwa umhifadhiwa katika hospitali hiyo pia.

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.