RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA CHIFU KINGALU
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepokea kwa mshtuko na majonzi
taarifa ya kifo cha Chifu wa Waluguru, Chifu Kingalu Mwanabanzi ambacho
kimetokea asubuhi ya leo, Jumatano, Julai Mosi, 2015 Kitengo cha Moyo
cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Katika
salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Dkt. Rajabu
Lutengwe, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea taarifa cha kifo cha Chifu
Kingalu kwa mshtuko na majonzi.
”Nimeshtushwa
na taarifa za kifo cha Chifu Kingalu ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea
asubuhi ya leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kwa hakika, kifo
hiki kimeifanya jamii yetu kupoteza kiongozi aliyeendesha shughuli zake
kwa busara kubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Binafsi nilimjua Chifu Kingalu katika maisha yake. Alikuwa kiongozi mwenye busara na aliyetetea mila na tamaduni za watu wake. Alikuwa kiongozi mpenda watu na aliyejali sana maslahi na matakwa ya wafuasi wake. Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro salamu zangu za rambirambi nikikupa pole kwa kuondokewa na mmoja wa viongozi wa kijamii katika eneo lako.”
“Aidha,
kupitia kwako nawatumia wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro na wanajamii
wa Kiluguru kwa kuondokewa na kiongozi wa tamaduni na mila zao. Vile
vile, nakuomba unifikishie pole zangu nyingi kwa wanafamilia ambao
wamepoteza mhimili wao. Naungana nao katika msiba huu ambao pia ni msiba
wangu. Naungana nao pia kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya
Marehemu Chifu Kingalu Mwanabanzi. Amina.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Julai,2015
Leave a Comment