MATAABIKO YA MSALITI BAADA YA USALITI!
MTENDWA wa usaliti hupata maumivu makali, wakati huohuo mwanzoni msaliti hukenua kwa kudhani ameshinda. Maisha hayapo hivyo!
Anayesalitiwa humwaga machozi kwa kilio cha mahangaiko ya moyo. Husahau kumshukuru Mungu. Hutamani kulipa kisasi. Hushindwa kutambua kuwa mzunguko wa maisha ya binadamu kama Maulana alivyoumba, tendo baya humrudia mtendaji mwenyewe wasaa unapotimu.
Laiti kila mmoja angejua mataabiko ambayo wasaliti hukutana nayo, kungekuwa na nafuu kubwa ya kimaisha. Idadi ya vitendo vya usaliti ingepungua.
Msaliti anapaswa kujua; Unapomsaliti mwenzio maana yake unakuwa sawa na kuyageuza maisha yake juu chini. Hilo siyo jambo dogo, kwani unaharibu mfumo wa maisha yake. Maumivu unayompa ni makubwa mno.
Katika uhusiano wa kimapenzi au ndoa, unapomsaliti mwenzio unakuwa umeingiza kaa la moto ndani ya moyo wa mwenzako. Aliwekeza upendo wake na imani kubwa, usaliti wako unamsababishia aende kuanza upya!
Wachumba wanaachana, ndoa zinavunjika. Yupo ambaye amewahi kutafsiri usaliti kama mfano wa mtu aliyetumia muda mrefu kujenga ghorofa lakini wewe unakuja kubomoa kwa siku moja.
Imani inajengwa na huchukua muda mtu kumwamini mwenzi wake kwa kiwango cha kutokuwa na shaka juu yake. Inapotokea anabaini kufanyiwa kitu tofauti na imani aliyokuwa nayo, kila kitu hubadilika. Imani yote huondoka na ni vigumu mno kumwamini tena.
UNAYAJUA MATAABIKO YA DAUD?
Daud ni mtu wa Mungu lakini alipofanya dhambi ya usaliti, alikutana na majanga makubwa. Jaribu kufikiria kama Daud pamoja na ukuu wake aliotakaswa na Mungu yalimfika, wewe mwenzangu na mimi je?
Ukweli ni kuwa matokeo ya kujirudia kwa vitendo viovu vya nyuma, hudhihirika kwa namna mbalimbali. Tatizo ni kuwa wahusika huwa hawajitokezi na kutoa ushuhuda. Nitaeleza!
Kabla ya kufika kwenye pointi ya kuchambua mateso kama siyo mataabiko ya wasaliti, tubaki kwenye kuyamulika mataabiko ya Daud.
Kwa kujivunia ufalme wake, Daud alimchukua mwanamke anayeitwa Bathsheba ambaye ni mke wa Uriah, aliyekuwa askari katika moja ya vikosi vyake.
Daud aliwatuma walinzi wake wakampeleka Bathsheba chumbani kwake, pamoja na kuambiwa kuwa huyo ni mke wa Uriah, bado hakurudi nyuma, akalala naye!
Baada ya kulala na Bathsheba, Daud akanogewa, akaamuru Uriah auawe akiwa kwenye uwanja wa mapambano. Maskini ya Mungu, Uriah aliponzwa na mkewe. Eti kosa lake ni kuwa na mke mzuri.
MUNGU ALIPOMKASIRIKIA DAUD
Katika Biblia Takatifu, Soma 2 Samuel 12, utaona mtiririko huu;
1. Ndipo Bwana akamtuma Nathan aende kwa Daud. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.
2. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana.
3. Maskini hakuwa na chochote, isipokuwa kondoo mmoja ambaye alimtunza sana.
4. Siku moja yule tajiri alipata ugeni. Akataka kumtengenezea kitoweo, badala ya kuchinja moja kati ya mifugo mingi aliyonayo, akaenda kumtwaa yule kondoo wa maskini.
5. Ndipo Daud akashikwa na hasira, akamwambia Nathan, huyo tajiri aliyemdhulumu mwenzake kondoo anastahili kuuawa kwa unyama aliofanya.
6. Daud akasema pia tajiri anapaswa kulipa fidia ya kondoo mara nne, kwa sababu alikosa huruma kwa maskini.
7. Basi Nathan akamwambia Daud, wewe ndiwe mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israel, asema hivi: “Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israel, nikakuokoa na mkono wa Sauli.”
8. Nathan anaendelea kumkariria Daud maneno ya Mungu: “Nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israel na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha.”
9. Nathan sasa anazungumza kumsema Daud; “Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uriah, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemuua huyo kwa upanga wa wana wa Amon.”
10. Ona sasa ahadi kali ya Mungu kama ilivyosemwa na Nathan: “Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uriah, Mhiti, kuwa mke wako.”
11. Nathan anaendelea kuisema adhabu kali kwenda kwa Daud kwa kitendo alichofanya: “Bwana asema hivi, angalia, nitakuondoshea kinga uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.”
12. Muogope Mungu, ona Daud mtu wa Mungu alivyoambiwa: “Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israel wote na mbele ya jua.”
13. Si una kiburi kuwa Mungu husamehe haraka? Hata Daud aliomba msamaha, alimwambia Nathan: “Nimemfanyia Bwana dhambi.” Nathani akamwambia Daud: “Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.”
14. Nathan akaendelea: “Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.”
15. Naye Nathan akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uriah alimzalia Daud naye akawa hawezi sana.
16. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daud akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini.
17. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi, lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.
18. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daud wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu, basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa?
19. Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong'onezana, Daud alitambua ya kuwa mtoto amekufa, basi Daud akawauliza watumishi wake, Je, mtoto amekufa? Nao wakasema, amekufa.
Nakatisha mistari ya Biblia ili uone namna ambavyo Daud alipata mataabiko. Dhambi ile ilileta madhara makubwa kupita kiasi.
Ukichimba zaidi, utagundua kuwa licha ya kusababisha uzinzi, pia yapo madhara mengine yaliyojitokeza. Kulitokea mauaji ya mtu asiyekuwa na hatia (Uriah). Jina la Bwana lilitukanwa kutokana na mpakwa mafuta wa Bwana (Daud) kuanguka katika dhambi.
Baada ya uzinzi ule, mtoto batili alizaliwa na vilevile akafa. Uasi ulitokea nyumbani mwa Daud na kusababisha aibu kubwa ya Absalom (mwana wa mfalme) kulala na wake za babaye, tena mbele ya kadamnasi ya Waisrael.
Kulitokea laana ya upanga kutoondoka katika nyumba ya Daud, ubakaji, mauaji na kadhalika. Yaani amani ilitoweka kabisa nyumbani mwa mfalme Daud. Rejea ahadi ya Nathan kama alivyotumwa Mungu amwambie Daud.
Kwamba yeye akiwa na wake wengi si alimtamani Bathsheba, mke pekee wa Uriah, na akaamuru auawe? Sasa naye wake zake walitembea na mwanaye Absalom. Tena mbele ya kadamnasi. Ni ile ahadi ya kuwa aibu hiyo itadhihirika mbele ya Israel yote. Huyu aliyetendwa hivi ni mpaka mafuta wa Bwana. Hasira za Mungu kwa mkimbilia mali za watu ni za kiwango gani?
Ni ukweli kuwa Mungu alikuwa na uwezo wa kumdhibiti Daud asifanye ushenzi kwa Bathsheba lakini bila shaka aliacha yatokee ili kudhihirisha mambo mawili makuu.
Mosi; Ni kuthibitisha kuwa binadam anabaki kuwa kiumbe dhaifu pamoja na kupakwa mafuta ya utakatifu.
Pili; Ionekane kuwa Mungu habagui, yeyote anayekosea atakutana na adhabu kali bila kujali nafasi yake
MALIPO NI DUNIANI
Chickens come home to roost; Hii ni methali ya Kiingereza yenye maana kuwa ubaya wowote ambao utaufanya, baadaye utakuja kukurudia.
Methali hiyo ina zaidi ya karne saba. Katika nahau hiyo, ubaya ambao mtu huufanya, unafananishwa na kuku, kwamba ni kawaida kuku hutoka kuzunguka akitafuta chakula lakini mwisho hurejea bandani.
Kwamba mtu anapofanya ubaya, huzunguka huku na huko lakini ipo siku ubaya wake utamrejea kwenye banda lake.
Msemo huo ulipata umaarufu mkubwa pale mwanaharakati Malcolm X, alipoulizwa maoni yake kuhusiana na kuuawa kwa Rais wa 35 wa Marekani, John Kennedy, aliyepigwa risasi. X alijibu: “Chickens come home to roost.”
Kwamba watawala walikuwa hawachukui hatua pale Waafrika walipouawa, kwa hiyo kifo cha Kennedy ni matokeo ya kufuga jipu la ukatili, kwa hiyo limewatumbukia wenyewe.
Ipo dhana ya Karma, ikianza kwenye imani ya Buddha, kuwa jambo lolote ambalo unalifanya leo, lina malipo yake. Ukitenda mema, wema wako utaukuta mbele ya safari. Ukifanya mabaya, hutajua siku lakini lazima utaukabili zamu inapofika.
DHAMBI HAIKIMBIWI
Harrison ni jaji, usiku mmoja akiendesha gari, taa ilimulika gizani na kuwaona watu wakimuua mwenzao. Bahati nzuri aliwatambua wote. Aliyeuawa ni James, wauaji walikuwa watatu, Larry, Jaden na Chris.
Baada ya wiki moja Harrison akiwa kazini alipangiwa kusikiliza kesi ya mauji ya James. Mtuhumiwa aliyeletwa mbele yake ni Jorum. Kumbuka kuwa Harrison kama jaji aliwaona wauaji. Lakini maadili ya kazi yake hayamtaki kusema alichokiona, isipokuwa kutoa hukumu kutokana na matokeo ya mwenendo wa kesi.
Kesi ilipofika wakati wa ushahidi, vilitolewa vizibiti vya nguvu kabisa kuonesha wazi Jorum ndiye aliyehusika na mauji. Mpaka ushahidi unakamilika hakukuwa na namna yoyote ya kumuokoa Jorum na hukumu ya kifo kutokana na mauaji ya James.
Harrison akawa anaumia mno, maana yeye aliwaona wauaji na anawajua. Anafahamu fika kuwa James hakuhusika na mauaji yale. Kilichomuumiza Harrison ni kuona kuwa anakwenda kumpa mtu adhabu ambayo hakuwa na hatia nayo. Ushahidi ulitengenezwa na umethibitisha kuwa Jorum ndiye alimuua James.
Siku moja kabla ya hukumu, Harrison alikuwa mwenye mawazo mno. Hukumu ya Jorum ilimtesa hasa. Mwisho aliamua kwenda gerezani ambako Jorum alikuwa amewekwa mahabusu.
Harrison akamwambia Jorum: “Najua kabisa wewe siye uliyemuua James.”
Jorum akajibu: “Ni kweli mheshimiwa, mimi naonewa. Hii kesi imetengenezwa.”
Harrison aliwaza kisha akamuuliza Jorum: “Bila kunificha kabisa, kabla ya tukio hili, wewe huko nyuma umewahi kuua?”
Jorum: “Ni kweli niliwahi kuua zamani lakini hakuna aliyejua.”
Harrison akasema: “Basi hukumu ya kesho nitaitoa kwa ajili ya yale mauaji ambayo uliua na hukujulikana. Nilikuwa napata shida kumhukumu mtu asiye na hatia, kumbe hatia unayo.”
Chukua hii; Unapokuwa kwenye kipindi cha maumivu, usilalamike sana kuwa unaonewa, nawe kumbuka uliyoyafanya nyuma. Kama uliwahi kuumiza wenzako pokea kuwa nawe muda wako umefika wa kuumia. Ndiyo maisha, ndivyo safari ya kiroho inavyokwenda.
Unapoingilia uhusiano wa watu kwa mabavu, ukijidaia fedha zako, tambua kuwa zipo adhabu za aina nyingi. Dunia siyo uwanja wa fujo kama wengine wanavyojidanganya, ipo nguvu isiyoonekana, ambayo huwalipia visasi waja wanyonge kwa namna ya kuumiza kabisa.
Bure alikuwa mume wa Justa. Bosi wa Bure anaitwa Kamau, naye akampenda Justa. Ili aweze kumfaidi vizuri Justa, Kamau alimhamisha Bure kituo cha kazi, alimtoa Dar es Salaam akampeleka Mwanza.
Kamau ana mke wake, kwa hiyo burudani zake na Justa zilikuwa mchana tu. Justa mumewe hayupo, usiku akaona siyo vibaya kumuingiza Francis chumbani kwake. Kamau akawa wa mchana na kuvuna pesa, usiku anakuwa na Francis, anamhonga na wanalala wote.
Bure akiwa Mwanza akajua kila kilichokuwa kinaendelea, akafanya taratibu za talaka, akaachana na Justa. Kumbe Francis ni mwathirika wa homa ya ini (Hepatitis B), alimwambukiza Justa ambaye naye alimpa Kamau. Na hivi mzunguko wao ulikuwa kwa mara kwa mara, maambukizi yalikuwa makali.
Wote watatu, yaani Francis, Justa na Kamau, walifariki dunia baada ya mateso makali ya kuugua kansa ya ini (liver cancer) na ini kuharibika (cirrhosis of the liver). Bure mpaka leo yupo, anadunda. Ana familia yake aliyoianzisha baada ya kuachana na Justa. Alipata kazi bora zaidi baada ya kuachana na kampuni ya Kamau.
Helen ana umri wa miaka 37 sasa, alishaapa kuwa hataolewa tena. Anadai wanaume hawaaminiki na hawatosheki. Pale alipo ana watoto wanne, kila mmoja ana baba yake. Alishaolewa ndoa tatu, zote zilivunjika kwa sababu ya kufanana.
Mtoto wa kwanza Helen alimpata alipokuwa na uhusiano na mume wa mtu anayitwa Kibuda. Mke wa Kibuda aliujua uhusiano kati ya Helen na mumewe na aliumia sana. Walishawindana mitaani mpaka kupigana.
Mke wa Kibuda alimuonya mno Helen kuachana na mume wake lakini haikuwezekana, matokeo yake Helen akazaa mtoto na Kibuda. Mwenyewe alisema alifanya vile kumkomoa mke wa Kibuda.
Siku zikapita Helen akampata Modest, wakafunga ndoa. Kipindi akiwa mjamzito, Helen alishtuka kugundua kuwa mume wake anatembea na housegirl. Ule mshtuko alioupta, alijifungua mtoto kabla ya siku zake, yaani njiti.
Ulipita muda, Helen akawa anaumia, mume wake kutembea na housegirl aliona kadhalilishwa.Pamoja na mtoto mchanga, alilazimisha apewe talaka. Ndoa ikavunjika, Helen aliondoka kwenye nyumba, housegirl akabaki anatawala.
Maisha ya kulea watoto wawili bila mume yalimtesa sana Helen. Mtoto alipokua, alipata mwanaume mwingine, Vincent, walikwenda bomani wakafunga ndoa. Walipata mtoto mmoja, akawa wa tatu kwa Helen.
Helen akagundua kuwa Vincent ana nyumba ndogo na kazaa naye, moto ndani ya nyumba uliwaka, wakaachana. Helen akawa mama pekee (single mother) akiwa na watoto watatu.
Umri unaenda, naye ana kiburi cha urembo, Helen baadaye akatua kwa mwanaume anayeitwa Bob. Huyu hata hawakufunga ndoa, waliamua kuishi tu.
Tatizo la Bob likawa ni kukosa uvumilivu anapoona mwanamke. Kila rafiki wa Helen alimtongoza, wengine alitembea nao, wapo waligombana na Helen. Walipata mtoto mmoja, akawa wa nne kwa Helen. Mwisho waliachana.
Siku zote Helen wimbo wake ni kuwalaumu wanaume kuwa baba yao ni mmoja, kuwa hakuna mwenye afadhali, kila aliyekutana naye amekuwa na vioja vya kipeke yake.
Ambacho Helen huwa hakumbuki ni makosa aliyoyafanya kwa Kibuda. Hakumbuki kama alimuumiza mke wa Kibuda. Hajui kuwa anavyotangatanga ndivyo ambavyo kuku wanarudi bandani (chickens come home to roost). Vilevile anatimiza ukweli kuhusu dhana ya Karma.
Lyndon ni mkurugenzi wa kampuni kubwa, anajulika na watu wanamheshimu kutokana na uwezo mkubwa kifedha. Kitu ambacho wengi hawakijui ni kuwa maisha yake ya kimapenzi yamejaa mateso makubwa.
Kutokana na jeuri ya fedha na ubosi wake, Lyndon amekuwa hachagui aina ya mwanamke wa kutembea naye. Wafanyakazi wa kampuni yake ambao ni wake za watu hutembea nao.
Ana mke pamoja na nyumba ndogo za kudumu tatu. Kote huko ni mateso kwake, kwani kila akipindua anagundua watu wanamlia vyake, yeye anahudumia watu wanakula bure. Kwa mkewe pia wasio na woga hupita.
Yeye ni kidume mpaka kwa wake za watu, lakini anateswa na jinsi vidume wenzake wanapoingia kwenye himaya zake na kumlia viota vyake, mbaya zaidi mpaka kwa mkewe. Anaishi kwa kuteseka, mara akodi wahuni kwa ajili ya kuwadhuru wale ambao anakuwa amewahisi wanaingia kwenye nyumba zake. Chickens come home to roost!
Umeoa? Heshimu ndoa yako, maana ukicheza faulo yoyote lazima malipo utayapata. Umeolewa? Hakikisha unakuwa mke bora. Ukijisahau, maisha yatakufundisha umuhimu wa kuwa mkweli kwenye ndoa.
Unaye mchumba? Hakikisha unakuwa mkweli kwake? Je, boyfriend au girlfriend? Husika kama ambavyo unatakiwa. Kila hatua ambayo unapiga ina malipo yake. Ukienenda vizuri, utalipwa mazuri, ukienda vibaya utapata unachostahili.
Kama wasemavyo kuwa ujana ni maji ya moto, wengi hudanganyika wakiwa vijana. Wanapoteza muda wao kutembea na wake za watu au waume za watu. Hujisahau pale ambapo wao wakiingia kwenye ndoa na kujikuta wanalipa gharama za matumizi mabaya ya ujana.
Chukua hii; Ukiwa kijana mzuri, unajiheshimu na unaziheshimu ndoa za wengine, Mungu atakupa mwenzi bora ambaye hatakuumiza, hatakusaliti na mtashirikiana kuifanya ndoa yenu kuwa mfano bora. Ndoa yenye upendo na maelewano!
Pokea na hii; Ukiwa kijana wa hovyo, hujiheshimu na unaingilia ndoa za watu bila woga. Elewa tu kuwa Mungu atakupa mwenzi msumbufu ambaye daima mtasumbuana, mtafumaniana, mtaumizana. Lazima kuku warejee bandani!
Bwire na Martha ni wanandoa na kila mmoja ana historia yake ya nyuma. Bwire alivunja ndoa ya watu, alipotembea na mke wa jirani yake. Martha amekuwa hodari wa kutoka na waume za watu mpaka alipotua kwa Bwire.
Martha na Bwire walipooana, walijidanganya kuwa wamekua na waliyoyafanya nyuma hayatawarudi. Martha akawa anapokea taarifa za wanawake wa nje wa Bwire. Martha akaona ujinga, akamlipizia, naye akawa anatoka nje hovyo. Alitembea mpaka na watu wa karibu na mumewe, tena mpaka kitandani kwake.
Bwire alipokuja kugundua ushenzi wa mkewe, moto uliwaka kisha wakaachana. Hawakujua kuwa Mungu aliwakutanisha ili waumizane kwa sababu ya malipo ya uhuni waliofanya kwenye ndoa za wenzao. Ukivunja ndoa ya mwenzako na yako itavunjwa tu! Kuku lazima arudi bandani.
Malcolm X kwa chuki yake dhidi ya usaliti, alisema: “To me, the thing that is worse than death is betrayal. You see, I could conceive death, but I could not conceive betrayal.”
Kiswahili: Kwangu, kitu kibaya kuliko kifo ni usaliti. Unaona, naweza kujenga fikra kuhusu kifo lakini siwezi kuupatia picha usaliti.
Mwandishi wa Kijapan, Mineko Iwasaki, naye alisema: “Stab the body and it heals, but injure the heart and the wound lasts a lifetime.”
Kiswahili: Uchome mwili kisu utapona, lakini jeruhi moyo na jeraha lake litaishi maisha yote.
Wote tunapaswa kuuogopa usaliti maana malipo ni duniani. Wote tuuchukie usaliti, maana unatuumiza sisi wenyewe.
KUMBUKA
MAISHA YANA MITIHANI MIKUBWA SANA JIFUNZE KUPITIA MITIHANI WANAYOPITIA WENZAKO ILI SIKU UKIKABILIANA NA MTIHANI WOWOTE ULE UJUE NI JINSI GANI YA KUWA MVUMILIVU NA KUWEZA KURIKABILI
Leave a Comment