NDOA YAKE YASABABISHA KIFO CHAKE
Ilikuwa ni Jumamosi tulivu,
sikuwa na kazi nyingi sana. Siku hiyo nilikuwa na miadi na mmoja wa wateja
ofisini kwangu kituo cha msaada wa Kisaikolojia HT&L CLINICAL THERAPY.
Mteja wangu alikuwa akiitwa
Claudia (sio jina lake halisi). Alikuja kwangu na kulalamika ni kwa jinsi gani
amegundua kuwa mumewe sio muaminifu na anatoka nje ya ndoa.
Alikuwa anahisi kusalitiwa
mno na alikuwa amechanganyikiwa, alikuwa akinielezea hali jinsi ilivyo huku
akitokwa na machozi. Nilijitahidi kumpa moyo na kumueleza kuwa haya yataisha.
Nikamuomba anipe namba ya
simu ya mumewe na nikamuahidi kukutana na wote, yeye na mumewe tuweze kupata
suruhisho la matatizo ya ndoa yao. Pia nikamhakikishia kwamba kwa Neema ya
Mwenyezi Mungu amani itarudi ndani ya ndoa yao.
Baada ya wiki moja niliweza
kuwasiliana na mumewe na hakuwa mkaidi alikuja ofisini kwangu na tukawa na
'session' pamoja yeye pamoja na mkewe. Baada ya maongezi ya kirafiki, alikubali
kwamba ni kweli anao mchepuko. Na amekuwa akichepuka mara kwa mara.
Alimtupia lawama zote mkewe
na kuniambia kwamba haya yote mpaka yeye kuchepuka nje na kutojali ndoa yake
amesababisha mke wake mwenyewe.
Akaniambia matatizo
yalianza pale dada wa mke wake yaani shemeji yake alipokuja kuishi nao.
Walikuwa na ndoa changa ndio kwanza ikikuwa. Kwa maneno yake alinisimulia;
" Tulikuwa tumepanga
chumba kimoja tu, na niliona si vema huyu shemeji yangu nae awepo kwenye chumba
kidogo kama kile"
"Tulikua tunahitaji
muda mrefu kidogo tukiwa peke yetu ili kujenga ndoa yetu changa bila kuingiliwa
na ndugu au mtu yeyote, hivyo dada wa mke wangu alitunyima kabisa uhuru wa mimi
na mke wangu kuwa pamoja"
"Shemeji yangu, yaani
dada yake na mke wangu alikuwa anao uhuru wa kupitiliza, aliingia tunakolala na
mke wangu, alikuwa akilala kitanda chetu muda wowote anapojisikia na alikuwa
haniheshimu hata kidogo hata mbele ya mdogo wake"
"Na kila nilipokua
nikimueleza mke wangu juu ya tabia za dada yake na kumsisitizia amwambie arudi
kwao, mke wangu alinijia juu na kuniambia nina mdharau ndugu yake, na kama
anataka aondoke basi na yeye ataondoka"
"Nilichanganyikiwa kwa
kweli, shemeji yangu alikuwa na kiburi, kila nikimueleza arudi nyumbani kwao
hakunisikia, nilishangaa mno kwa nini alikua aking'ang'ania kukaa nasi kwenye
chumba kimoja na huku ndoa yetu ikiwa ndio kwanza ipo changa"
"Mara ya mwisho mimi
kumgusia hilo suala, ilikuwa ni siku ambayo mke wangu aliniambia mbele ya dada
yake kwamba dada yake hataenda sehemu yoyote. Sikuweza kuvumilia, ukizingatia
nilikuwa nimekaa kama miezi miwili hivi bila kushiriki tendo la ndoa."
Sikuweza kuvumilia kwa
kweli, nilivaa viatu vyangu nikatoka. Sikuwa na uelekeo maalumu, nilizunguka
zunguka tu mpaka nikafika Bar fulani iliyo nje ya mji kdogo. Nilikaa katika
hiyo Bar nakuanza kunywa bia, pembeni yangu alikaa dada mmoja ambae alikuwa
mrembo kweli"
"Nilimkaribisha mezani
kwangu, tulikunywa sana bia pamoja na baadae nikachukua chumba pale pale maana
Bar ilikuwa na vyumba pia. Niliingia nae na nikafanya nae mapenzi"
"Na hapo ndipo
nilipoanza kuchepuka, yule dada niliyekuatana nae pale Bar alikuwa akiitwa
Diana (sio jina lake halisi). Na alikuwa akiishi bagamoyo. Tukatokea kupendana
sana. Nikawa nikisafiri kwenda Bagamoyo. Mara nyingi nilichelewa kurudi
nyumbani au siku nyingine nikawa sirudi hata siku mbili tatu hata wiki"
Mume wa yule dada alinipa hayo maelezo yake.
Kwa kufupisha story, baada
ya kumsikiliza huyu mume japo mke alikuwa amepanick, mimi niliongea nao
maongezi ya kina, niliwaonesha maandiko ya Mwenyezi Mungu yanasema nini juu ya
Ndoa na nikawaeleza hasara za yeye mume kuendelea kuchepuka, huku akiacha mkewe
wa ndoa. Pia nikampa mbinu za kufanya ili shemeji yake aweze kuondoka pale
nyumbani kwake.
Mke nae nilimueleza umuhimu
wa mume wake hasa kipindi hiki ndoa ikiwa bado changa na ikihitaji jitihada za
wote wawili. Na kumsisitizia aruhusu dada yake aondoke.
Walinielewa na nilifurahi
kwa kuwa mume aliniahidi kurudi kwa mkewe na kuendeleza ndoa yao changa.
Ndugu msomaji, kama
mchekeshaji maarufu hapa Tanzania Mjuni Mpoki alivyoimba katika kibao chake kimoja
kwamba "Mapenzi yana nguvu kuliko hata breakdown." msemo huo
ulijidhihirisha kwani yule mume, baada ya kukaa siku chache tu na mke wake
alirudi Bagamoyo kwa mchepuko wake, ingawa shemeji yake yaani dada wa mkewe
aliondoka na kuwaachia uhuru.
NA NDIPO JANGA LILIPOTOKEA!
Usiku mmoja mkewe ambae
alikuwa na pumu (asthma) akiwa peke yake, wakati bwana mkubwa yupo kwa mchepuko
wake Bagamoyo, pumu ilimbana sana, Blood pressure (BP) ililuwa juu, sauti
haikuwa inamtoka, alihangaika sana na mwishoe akafariki kutokana na hiyo attack
(shinikizo)
Ndio alifariki kifo cha
maumivu mno pasina msaada wowote, aheri hata angalikuwepo mtu yeyote ndani
huenda angaliweza kutoa msaada wa haraka wa kumuwahisha hospitali!
_____________________________________________
Sote tunapaswa tujifunze
kuweka ndoa zetu au mahusiano yetu mstari wa mbele, panapokuwa na mapenzi ya
kweli na heshima kwa kila mmoja wetu, hali kama hiyo hapo juu haiwezi
kujitokeza na hata ikitokea basi huamuliwa kwa busara na matokeo hua ni chanya.
Sio hasi kama yaliyotokea katika simulizi hapo juu.
Sasa tusemeje?
- Je Mwanamke
alijisababishia kifo chake mwenyewe?
- Mume wake ndio alikuwa
chanzo cha kifo chake?
- Ni kweli mke wake
alipaswa kulaumiwa kwa yeye kuanza kuchepuka?
- Au tumlaumu dada mtu kuja
kukaa kwa shemeji yake na huku akijua wanaishi chumba kimoja tu?
Toa maoni yako hapo chini.
Ndoa sio mchezo, ndoa sio
masihara, if you mess up with marriage it might be the way to your grave. Be
wise and pray to God
Leave a Comment