Tabia 10 ambazo husababisha UMASKINI






Kila mtu huwa na malengo, kila mwenye malengo hutamani yafanikiwe. Hatahivyo watu wengi hufeli kutimiza malengo haya. Takwimu zinaonesha kati ya watu takribani Bilioni 7.7 waliopo duniani ni asilimia 5 tu kati yao ambao ni matajiri ambao utajiri wao huweza kurithiwa na vizazi vyao vinavyowafuata.
Asilimia 15 kati yao ni wale wa uchumi wa kati, ambao maisha yao ni ya kawaida, wanaweza kupata mahitaji yote muhimu ya maisha huku asilimia 80 ya watu wote duniani ni maskini yaani wanategemea kufanya kazi na kupata fedha zinazoweza kuwakimu kwa siku au wanategemea msaada kutoka kwa serikali za nchi zao.
Kutokana na hili wataalamu wa uchumi wameeleza kuwa zipo tabia ambazo watu huziona za kawaida lakini tabia hizi husababisha umasikini. brunokimaro.blogsopt.com inakuletea orodha ya tabia hizo kama ifuatavyo.
1. Kutumia muda mwingi kuangalia TV, sinema au tamthiliya
Dalili moja ya mtu kuwa masikini siku za mbeleni inatajwa kuwa utaratibu wa kutumia muda mwingi kuangalia TV badala ya kufanya shughuli za kuingiza kipato au hata shughuli za ziada zenye kuongeza manufaa fulani hata kama sio pesa moja kwa moja.
Masaa mengi unayotumia kuangalia TV unaweza kuyatumia kufanya shughuli za kibunifu, na kuutengenezea thamani muda wako. kuangalia TV sio jambo baya lakini kutumia masaa mengi kuangalia TV, sinema au tamthiliya ni hasara.
2. Kununua chakula (Fast food)
Hii ni tabia nyingine ambayo inatajwa ambayo kama hairekebishwi hupelekea umaskini. Kama haukumbuki ni lini ulipika mwenyewe nyumbani kwako kwasababu unanunua chakula wakati wote basi hiyo ni dalili mbaya.
Kwanza chakula cha fast food, kama pizza, burger, chipsi na vinginevyo huwa na mafuta mengi na husababisha magonjwa kama uzito uliopitiliza, magonjwa ya moyo n.k.
Haya yote hupunguza ufanisi wa mtu kufanya kazi vizuri ili afanikiwe au afikie malengo yake. Madhara haya huathiri maeneo yote maisha, kiuchumi, kiakili, kijamii na hata kimahusiano.
Tofauti na hilo, kununua vyakula hivi husababisha matumizi ya pesa makubwa ambayo yanaweza kuepukika. Kwa mfano kama pizza moja ni sh elfo 20, mtu anaweza kutumia robo au theluthi ya pesa hiyo kununua chakula na kupika mwenyewe mlo kamili yaani balanced diet.
3. Kuchelewa kuamka
Tabia hii kufanyika katika umri wa ujana inaelezwa kuwa ni dalili ya kuukaribisha umaskini katika siku za mbeleni.
Vijana ambao wanakuwa wazembe kufanya kazi kwa bidii kwenye kipindi chao cha ujana, hufanya kazi zaidi na kwa tabu wakifika umri wa kuanzia miaka 40 tena yawezekana bila malipo makubwa, na hii ni kwasababu hawakutumia vizuri muda wao wa ujana kufanya kazi na kuwekeza kwa ajili ya miaka ya mbeleni.
Inaelezwa kuwa watu matajiri, kama Bill Gates, Elon Musk, Mark Zuckerberg na wengine, huamka mapema na kuanza kufanya kazi zao kwa bidii kila siku, sasa kama matajiri ambao utajiri wao ni endelevu, wanaona umuhimu wa kuamka mapema na kufanya kazi, vipi kuhusu kijana anayeanza kutafuta maisha?
4. Kulaumu wengine kwa matatizo unayopitia
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa moja ya tabia zinazoweza kumfanya mtu awe maskini ni pamoja na kulaumu watu wengine kutokana na kutofanikiwa kwako.
Kuna msemo unaosema “Maisha ni jinsi unavyoamua kuyaona” hivyo kila jambo linaweza kuwa ni la manufaa kwako aidha liwe zuri au baya, kinafanya utofauti kati ya hayo mawili ni jinsi utakavyoamua kulichukulia.
Jambo baya likitokea, masikini huwa wahanga wa jambo hilo lakini matajiri hulitafakari, na kuangalia sababu halisi ya jambo hilo kutokea kisha kuhakikisha halitokei tena au likitokea haliwaathiri au hata kuhakikisha wanatumia fursa yoyote inayopatikana katika janga hilo ili kunufaika nalo.
5. Kutoweka akiba
Akiba ni jambo la msingi sana katika mapato yoyote yanayopatikana. Akiba ya pesa husaidia pindi likitokea tatizo, inaweza kuwa ugonjwa, safari ya dharura na kadhalika. Kama huna akiba likitokea tatizo itakubidi uuze mali yako yoyote au uchukue mkopo ili kutatua tatizo hilo.
Tofauti na kutokea kwa matatizo, kama umeweka akiba na ikatokea fursa ya wewe kutumia pesa ili kuingiza faida, utanufaika kuliko mtu asiye na akiba, na huo ndio uzuri wa kutunza akiba ya pesa.
6. Kufanya manunuzi yasiyo kwenye mpangilio.
Hii ni pamoja na kununua vitu ambavyo havikuwa kwenye bajeti au mpangilio. Kutokana na hili, wataalamu wanashauri kufanya manunuzi ukiwa tayari umeandika orodha ya vitu unavyotaka kununua na sio kwenda sokoni au dukani na kuangalia kilichopo ili ufanye manunuzi.
Pia ni kama kuchukua mkopo ili kununua vitu ambavyo havizalishi pesa, kama kuchukua mkopo kununua furniture za ndani, au gari la kutembelea na vinginevyo. hiyo ni hasara na hupelekea umasikini.
7. Kuzaa watoto wengi
Kama wewe ni kijana na una mpango wakuja kuwa na familia yenye watoto wengi, hakikisha hali yako ya uchumi iko imara kabla haujaanza kuzaa watoto hao.
Wataalamu wanaeleza kuwa kipato kikiwa kidogo na watoto wakiwa wengi kwenye familia, kiwango cha umasikini kinaongezeka kwenye familia hiyo.
Inaelezwa kuwa matajiri wengi duniani, hawana watoto wengi japo kuwa wanauwezo kifedha na wangeweza kuwahudumia, wanajua ni gharama kuwapa watoto mahitaji yao yote ya msingi, tena kwa wakati.
Tajiri mkubwa duniani Bill gates ana watoto watatu, tajiri mwingine Warren Baffet ana watoto 3, Mark Zuckerberg ana watoto wawili, na kutokana na utajiri walionao, wanao uwezo wa kuwa na watoto zaidi ya watano.
8. Kutopima afya mara kwa mara
Inawezekana ukaona sio suala la msingi kupima afya mara kwa mara lakini hili ni suala la msingi kwa watu matajiri, kwani kuishi ukiwa na uhakika wa afya ndio msingi wa kuishi maisha ya mafanikio.
Kupima afya mara kwa mara kunasaidia kujua mapema kama una ugonjwa unaoanza mwilini mwako, hii ina faida kwani uwezekano wa kutibiwa na kupona kabisa kwa ugonjwa huo ni mkubwa zaidi lakini pia gharama utakazotumia kwa ajili ya matibabu zitakuwa nafuu kuliko ambazo zingetumika wakati ugonjwa umekuwa mkubwa.
Ni kama ilivyo kwa ugonjwa wa saratani, kujua mapema ndio uhakika kwa ugonjwa huo kutibiwa na kupona mapema tofauti na ukiwa umekomaa, au hata ugonjwa wa kifua kikuu, au figo na magonjwa mengineyo.
9. Kutumia pesa kabla ya kuzipata
Kama una tabia ya kukopa pesa kipindi ambacho hauna pesa huku ukitarajia kuzilipa pindi utakapopata pesa, hiyo ni dalili ya umaskini kukunyemelea.
Kuepuka athari hii wataalamu wanashauri kufanya kazi kwanza na kupata pesa kisha uendelee na kufanya matumizi ambayo unayahitaji.
10. Kuwa na marafiki wasio na malengo makubwa
Marafiki huweza kukusaidia kufikia malengo yako uliyojiwekea, lakini pia huweza kufanya usifikie malengo yako hayo.
Inashauriwa kuwa kama unataka kufanikiwa hakikisha unatumia muda mwingi zaidi na marafiki ambao wana malengo makubwa ya maisha, wanawaza mambo chanya na sio mambo hasi muda wote, ambao wanakukumbusha kufanya vitu vya msingi.
Hii inaweza kuwa kutunza muda, kutokata tamaa kwenye malengo yako au kuwa mbunifu zaidi, na hata kukukosoa kwa tabia ambazo zinarudisha nyumba maendeleo yako.

No comments

Theme images by sbayram. Powered by Blogger.